Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais Algeria, Abdelmadjid Tebboune anaongoza
-
Abdelmadjid Tebboune (wa pili kutoka kushoto) na wagombea wenzake
Matokeo ya awali ya uchagauzi wa rais nchini Algeria yanaonesha kuwa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Abdelmadjid Tebboune anaongoza baada ya kuwapiku wagombea wenzake wanne.
Ripoti zinasema kuwa, matokeo hayo ni kwa mujibu wa kura zilizokwisha hesabiwa katika mikoa mingi ya Algeria na kwamba Tebboune anaongoza kwa kupata kura nyingi zaidi.
Abdelmadjid Tebboune ambaye alikuwa waziri mkuu wa Algeria kuanzia mwezi Mei hadi Agosti mwaka 2017 ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kwamba, takwimu za vituo vya kupigia kura katika miji mbalimbali ya Algeria zinaonesha kuwa, anaongoza kwa kupata kura nyingi zaidi.
Waziri wa zamani wa utalii wa Algeria, Abdelkader Bengrine anashika nafasi ya pili akifuatiwa na Ali Benflis aliyekuwa waziri mkuu wa Algeria baina ya mwaka 2000 na 2003.
Uchaguzi wa rais nchini Algeria ulifanyika jana Alkhamisi katika anga ya mzozo na mvutano mkubwa kutokana na wananchi wa nchi hiyo kugawanyika katika makundi mawili ya wanaopinga na wanaounga mkono kufanyika uchaguzi huo.
Waalgeria wengi wamesusia uchaguzi huo wakisema wagombea wote ni wanasiasa wenye mfungamano na utawala za rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika unaohusishwa na ufisadi mkubwa na utendaji mbaya.
Uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika nchini Algeria tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika alipolazimika kung'atuka madarakani Aprili Pili mwaka huu kutokana na maandamano ya upinzani ya wananchi.