Mapigano yaibua wimbi jipya la wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoelekea Ethiopia
Mapigano baina ya wanajeshi katika eneo la Maiwut la Sudan kusini yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi kuingia katika jimbo la Gambella, Ethiopia.
Shirika la Ulinzi na Misaada ya Haki za Binadamu la Ulaya ECHO, limesema, tangu mwezi uliopita, kituo cha kupokea wakimbizi cha Pamdong kimepokea wakimbizi zaidi ya elfu 3.6. ECHO pia imesema, kutokana na ongezeko la wakimbizi katika kituo hicho, shirika hilo linahitaji fedha zaidi katika sekta zote ili kuwapatia misaada ya kibinadamu. Wakimbizi kutoka Sudan Kusini walianza kuingia nchini Ethiopia mwaka 2013 muda mfupi baada ya vita vya ndani kuanza huko Sudan Kusini. Mpaka sasa Umoja wa mataifa unakadiria kuwa Wasudan Kusini milioni 4 wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.
Haya yamearifiwa katika hali ambayo, Jumanne wiki hii Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alisema, yeye na aliyekuwa kiongozi mkuu wa waasi Riek Machar wamefikia makubaliano ya kuunda serikali iliyokuwa ikingojewa kwa muda mrefu ya umoja wa kitaifa. Kiir na Machar, ambaye sasa ni kiongozi wa upinzani, walikutana kwa muda wa siku tatu katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba, kuyatafutia ufumbuzi masuala makuu yanayozozaniwa na pande mbili, ambayo yalikwamisha kuundwa serikali ya mseto katika muhula uliokuwa umewekwa wa tarehe 12 ya mwezi uliopita wa Novemba. Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.