30 wauawa na kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila Nigeria
Kwa akali watu 12 wameuawa kwenye mapigano baina ya makabila mawili katika jimbo la Cross River kusini mwa Nigeria mpakani na Cameroon.
Duru za habari zinaarifu kuwa, mbali na watu 12 kuuawa, wengine 18 wamejeruhiwa katika makabiliano hayo baina ya makabila ya Ebom na Usumutong katika jimbo la Cross River.
Kadhalika nyumba nyingi zimechomwa moto katika vita hivyo, huku wakazi wa viijiji vilivyoshuhudia ghasia hizo wakikimbia makazi yao kwa hofu ya kushambuliwa.
Kamanda Mkuu wa Polisi wa jimbo la Cross River, Nkereuwem Akpan amethibitisha kutokea mapigano hayo, ingawaje hakutoa taarifa kamili kuhusu idadi ya vifo. Ameongeza kuwa, vikosi vya usalama vimetumwa kwenye eneo hilo kudhibiti mambo.
Mapigano kati ya makabila hayo hutokea mara kwa mara katika eneo hilo la Cross River. Makumi ya watu walipoteza maisha katika mapigano mengine ya kikabila katika jimbo hilo mwaka jana, mbali na nyumba nyingi kuchomwa moto.
Aidha mwezi Oktoba mwaka jana, watu 55 waliuawa katika mapigano mengine ya kikabila katika jimbo la Kaduna la kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.