Mustakbali wa Algeria baada ya kuapishwa rais mpya
Baada ya kupita miezi mingi ya mgogoro wa kisiasa na maandamano ya wananchi, hatimaye uchaguzi wa rais umefanyika nchini Algeria na Abdelmadjid Tebboune amechaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Wiki moja baada ya uchaguzi huo uliokuwa na "kaskash" nyingi, hatimaye Tebboune ameapishwa kuwa rais rasmi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Kaulimbui kuu ya Tebboune katika kampeni zake za uchaguzi ilikuwa ni kuanzisha mazungumzo na pande nzote nchini humo na kulifanya suala la Palestina kuwa ajenda na msingi mkuu katika siasa za nje za Algeria.
Abdelmadjid Tebboune ameapishwa kuwa rais wa Algeria katika hali ambayo, wananchi wengi wa nchi hiyo wameususia uchaguzi huo wakisisitiza kuwa, wagombea wote walikuwa ni mabaki ya utawala uliopinduliwa na wananchi wa Abdelaziz Bouteflika. Hata hivi sasa pia wananchi wengine wa Algeria wanamuona Tebboune kuwa ni muendelezo wa utawala ule ule wa miaka 20 iliyopita wa Bouteflika.
Hata hivyo baadhi ya wanasiasa na wananchi wa Algeria wanaamini kuwa, ijapokuwa Tebboune aliwahi kuhudumu katika utawala wa Bouteflika, lakini ameonyesha uwezo wa kutatua matatizo ya kijamii na kisiasa ya nchi hiyo. Wanasema, kama ambavyo wakati wa utawala wa Bouteflika, Tebboune alikuwa akiwakosoa vikali baadhi ya wanasiasa, hivi sasa pia anaweza kuvutia hisia za wananchi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa, kufungua milango ya uhuru wa kujieleza bali hata uhuru wa vyombo vya habari na hivyo kuwakosesha cha kusema wapinzani wake.
Hivi sasa rais mpya wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune ameahidi kufanya mabadiliko ya kimsingi nchini humo. Amesisitiza kuwa ameshikamana vilivyo na mageuzi yanayotakiwa na wananchi wa Algeria. Amesema: Nimeshikamana vilivyo na msimamo wangu wa kuwaletea wananchi wa Algeria mageuzi wanayotaka na ninao uwezo wa kufanya hivyo. Tebboune amenza kipindi cha urais wake katika hali ambayo, Algeria hivi sasa ina changamoto nyingi nzito. Anachopaswa kufanya rais huyo mpya mbali na kutatua matatizo ya ndani na nje, avithibitishie vyama vya upinzani kuwa, utawala wake ni tofauti kabisa na ule wa Abdulaziz Bouteflika tena katika mazingira ambayo hivi sasa Algeria inapitia kipindi kigumu mno cha migogoro mizito ya kisiasa na kiuchumi ya ndani na uingiliaji wa madola ajinabi.
Mizozo na hitilafu baina ya vyama na makundi ya kisiasa ya ndani ya Algeria bado zinaendelea. Sasa moja ya kazi kubwa zinazopaswa kutiliwa hima na serikali mpya ya nchi hiyo ni kuunganisha makundi ya kisiasa na kuleta mazingira mazuri ya mazungumzo na maelewano ya kuwezesha kutatuliwa matatizo mengine mengi yaliyopo nchini humo hivi sasa.
Noureddine Bekis, mhadhiri wa elimu jamii wa Chuo Kikuu cha Algiers anasema: Tebboune hana chaguo jingine isipokuwa kufanya mazungumzo na wapinzani wake wa kisiasa. Lakini hilo halitowezekana hadi pale atakapoweza kuwakinaisha wananchi na kuwawekea wazi siasa zake kuhusu maendeleo na hali iliyopo hivi sasa Algeria.
Miongoni mwa changamoto nzito za kiuchumi zilizoko Algeria hivi sasa ni mfumuko wa bei za bidhaa, umaskini na ukosefu mkubwa wa ajira. Pato la fedha za kigeni la nchi hiyo limeporomoka kutokana na kuanguka bei ya mafuta katika soko la dunia. Ufisadi na ubadhirifu serikalini ni kilio kingine kikubwa cha wananchi wa Algeria.
Tukija upande wa siasa za kigeni pia, rais mpya wa Algeria ameahidi kulipa kipaumbele suala la Palestina. Hata hivyo suala hilo pia lina changamoto nyingi hasa kutokana na jinsi nchi za Magharibi hususan Ufaransa zinavyoiangalia kwa jicho maalumu Algeria.
Hata hivyo, Sabri Boukadoum, waziri wa mambo ya nje wa Algeria amesema, nchi yake ina uwezo wa kutosha wa kutatua mambo yake bila ya msaada wa madola ya kigeni wala kukubali kubebeshwa mambo isiyoyataka.