Macron akiri ukoloni wa Ufaransa Afrika ulikuwa kosa kubwa, wapinzani wampinga
Baada ya Rais Emmanuel Macron kukiri hadharani kuwa ukoloni wa Ufaransa barani Afrika ulikuwa kosa kubwa, kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia chenye chuki za kikabila nchini Ufaransa amelalamikia msimamo huo wa Macron na kudai eti unatia doa historia ya Ufaransa.
Shirika la habari la Sputnik limemnukuu Marine Le Pen, kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha mrengo wa kulia cha National Assembly cha Ufaransa akisema katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Macron ameangalia upande mmoja na hasi tu wa "mchakato tata" akikusudia ukoloni, katika historia ya Ufaransa.
Akiwa nchini Ivory Coast, Macron alisema jana Jumapili kwamba, ukoloni wa Ufaransa barani Afrika ulikuwa kosa kubwa na kwamba yeye hatoki kwenye kizazi cha kipindi cha ukoloni wa nchi hiyo ya Ulaya.
Wanasiasa wengine wa Ufaransa wenye misimamo mikali na chuki dhidi ya wageni nao wamelalamikia vikali matamshi hayo ya Macron.
Hata mwezi Februari 2017 pia, wakati Emmanuel Macron alipokuwa mgombea wa urais wa Ufaransa alisema kuwa, ukoloni ni jinai dhidi ya binadamu.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, kumbukumbu chungu ya kihistoria iliyopelekea wananchi wa bara la Afrika, wanaharakati na hata wanasiasa wa bara hilo kutokuwa na mtazamano mzuri kuhusu madola ya kikoloni kama vile Ufaransa, Uingereza na kadhalika ndiko kulikoifanya serikali ya Paris itafute mbinu mpya yaani kulaani jinai za wakoloni ili kulinda ushawishi wao barani Afrika.