Tahadhari kuhusu kubadilika Libya na kuwa tishio kwa Afrika
Rais wa Nigeria ametahadharisha kuhusu athari za ukosefu wa amani huko Libya na kubadilika suala hilo kuwa tishio kwa usalama wa bara la Afrika.
Rais Muhammad Buhari wa Nigeria amesisitiza kupitia hotuba aliyoitoa katika bunge la Ulaya kuwa hali ya mambo kusini mwa Libya imeshindikana kudhibitika na kwamba kuingizwa kwa wingi silaha mchini humo kumelifanya eneo hilo kuwa soko la kununua na kuuzia silaha haramu. Rais wa Nigeia amelitaja jambo hilo kuwa hatari kubwa kwa usalama wa nchi za Kiafrika.
Baada ya kuangushwa utawala wa dikteta Muammar Gaddafi huko Libya mwezi Oktoba mwaka 2011, vinara wa kundi la kigaidi la Daesh waliainisha nchi hiyo kuwa mahala salama kwa ajili ya kuasisi kambi za kijeshi na kuingia katika nchi nyingine za bara hilo. Katika hatua ya kwanza tishio hilo lilizijumuisha nchi jirani na Libya kama Tunisia na Algeria. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa wanamgambo wa kundi la Daesh ambao wamepoteza udhibiti wa maeneo mengi ya ardhi ya Iraq na Syria hivi sasa wamezidisha harakati zao za kusonga mbele kijeshi huko Libya. Wasiwasi mkuu uliopo ni huu kuwa viongozi wa kundi la kigaidi la Daesh wameazimia kuyatwaa maeneo tajiri kwa mafuta kama vile Ras Lanuf na hivyo kujidhaminia pato kubwa la mamilioni ya dola zitokanazo na uuzaji mafuta.
Hatua ya kundi la Daesh ya kuasisi kambi ya kijeshi katika mji wa Sirte huko Libya na kutishia kuwa litazidisha mashambulizi yake dhidi ya taasisi za mafuta za nchi hiyo, yote hayo yameweka wazi lengo la kundi hilo la kujiimarisha kijeshi nchini humo. Kuwepo hofu na wasiwasi wa kujiri mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya makundi hasimu ya wanamgambo huko Libya wanaowania madaraka ya kisiasa kumeandaa uwanja wa kuingia na kujiimarisha zaidi wanamgambo wa Daesh barani Afrika. Hatari ya kusonga mbele kundi hilo hivi sasa imezitia hofu na wasiwasi nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kama vile Mali na Nigeria. Sababu hiyo imemfanya Rais Muhammad Buhari wa Nigeria kutahadharisha kuhusu kubadilika Libya na kuwa tishio kuu kwa usalama wa nchi za Kiafrika. Tahadhari hiyo imetolewa kufuatia kundi la Daesh kuwaajiri raia maskini kutoka baadhi ya nchi za Kiafrika kama Chad, Sudan na Mali kwa ajili ya kupigana, hatua ambayo itazidisha hali ya wasiwasi.
Wakati huo huo John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani hivi karibuni alidai kuwa mapambano ya muungano wa kimataifa dhidi ya Daesh yanapaswa kushadidishwa katika kukaribia uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa huko Libya. Weledi wa mambo waliwahi kutabiri kuwa nafasi ya kijiografia ya Libya pambizoni mwa bahari ya Mediterania italipelekea kundi la kigaidi la Daesh nchini humo kuwa tishio kwa biashara na usalama wa nchi za kusini mwa Ulaya. Tishio hilo awali lilizihusu zaidi nchi za kusini mwa bara la Ulaya kama Italia na Uhispania na kwa kiasi fulani Ufaransa. Tishio hilo la Daesh limekuwa kisingizio tosha kwa viongozi wa Ufaransa kuandaa utangulizi wa kuingilia kijeshi huko Libya.
Stephane Le Foll msemaji wa serikali ya Ufaransa amesema uwezekano wa nchi yake kuingilia kijeshi Libya utategemea masharti matatu ambayo ni kuundwa serikali ya umoja wa Kitaifa huko Libya, ombi la serikali ili Ufaransa iweze kuingillia kijeshi na kuwepo mawasiliano kati ya jamii ya kimataifa na Ufaransa. Weledi wa mambo wanaona kuwa masharti hayo ya Ufaransa hueda yakaandaa uwanja wa kuzuka mapigano mapya huko Libya. Sisitizo la Ufaransa la kutolewa kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaonekana kutokuwa na msingi kwa sababu karibu miaka mitatu iliyopita vikosi vya nchi hiyo vilitumwa kaskazini mwa Mali bila ya idhini ya baraza hilo. Wasiwasi uliobainishwa na John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani pia una lengo la kwatia hofu viongozi wa nchi za Kiafrika ili baadaye waafiki uingiliaji kijeshi wa Magharibi huko Libya.