Sudan yasaini makubaliano ya amani na kundi la waasi la SPLM-N
Baraza la Utawala la Sudan limesaini mapatano ya awali ya amani na kundi moja la waasi, ikiwa ni juhudi za kurejesha utulivu nchini humo.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo ya awali ilifanyika jana Ijumaa mjini Juba baina ya wawakilishi wa serikali ya Khartoum na kundi la waasi la Sudan People’s Liberation Movement-North (SPLM-N), chini ya upatanishi wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.
Baada ya kusaini makubaliano hayo, Naibu Mkuu wa SPLM-N, Yasir Said Arman amesema "hii ni hatua ya mwanzo, tutakamilisha mchakato huu na utawala mpya wa Khartoum hivi karibuni.
Huko nyuma pia, Sudan ilifikia makubaliano na kundi moja la waasi wa Darfur linalojiita Jeshi la Ukombozi wa Sudan ikiwa ni katika kalibu ya mwafaka wa amani ya Darfur uliotiwa saini mjini Doha Qatar.
Mazungumzo ya amani baina ya Baraza la Utawala nchini Sudan na makundi ya waasi yalianza Oktoba mwaka jana na yalitazamiwa kufikia tamati Disemba ili kurejesha utulivu nchini humo.
Serikali mpya ya Sudan inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kuboresha uchumi wa nchi hiyo uliosambaratika vibaya, kupambana na ufisadi, na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kurejesha amani katika maeno yote ya nchi hiyo.