Wanajeshi wa Sudan waanza kuondoka taratibu nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59054-wanajeshi_wa_sudan_waanza_kuondoka_taratibu_nchini_yemen
Waziri wa Utamaduni na Habari wa Sudan amesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wameanza kuondoka taratibu nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2020 02:53 UTC
  • Askari wa Sudan waliouawa Yemen
    Askari wa Sudan waliouawa Yemen

Waziri wa Utamaduni na Habari wa Sudan amesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wameanza kuondoka taratibu nchini Yemen.

Feisal Mohamed Salih ambaye alikuwa akizungumza pambizoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa amesema kuwa, Khartoum imefikia natija kwamba, mgogoro wa Yemen hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi na kwa msingi huo imenza kuwaondoa wanajeshi wake katika nchi hiyo. 

Waziri wa Utamaduni wa Sudan ameongeza kuwa, pande kadhaa zimebadili msimamo wao kuhusiana na vita vya Yemen, zikiwemo nchi waanzilishi wa muungano wa vita dhidi ya taifa hilo unaoongozwa na Saudi Arabia. 

Awali Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan  Abdallah Hamdok alikuwa amesema kuwa, nchi hiyo imepunguza idadi ya wanajeshi wake wanaopigana nchini Yemen kutoka askari elfu 15 hadi elfu 5. 

Askari wa Sudan wanauawa ovyo nchini Yemen

Tangu mwezi Machi mwaka 2015 Sudan ilitangaza kuwa inashiriki katika muungano wa vita wa Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen. Maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na hujuma na mashambulizi ya muungano huo. 

Maelfu ya askari mamluki wa Sudan pia wameuawa katika vita vya Yemen, suala ambalo limezusha upinzani mkubwa ndani ya Sudan kwenyewe ambapo vyama na makundi ya kiraia yanaishinikiza serikali iwarejeshe nyumbani wanajeshi wa nchi hiyo wanaopigana vita kwa niaba ya Saudi Arabia na Imarati.