Rais wa Ivory Coast abadili msimamo, asema hatogombea tena urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59569-rais_wa_ivory_coast_abadili_msimamo_asema_hatogombea_tena_urais
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast amesema hatagombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 05, 2020 22:56 UTC
  • Rais wa Ivory Coast abadili msimamo, asema hatogombea tena urais

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast amesema hatagombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika hotuba yake kwa Bunge katika mji mkuu wa nchi hiyo Yamoussoukro, Rais Outtara amesema, "nimeamua kuwa sitokuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 31 na nitakabidhi madaraka ya nchi kwa kizazi kipya."

Kauli hiyo ya Rais Outtara ambayo imepokewa kwa shangwe ndani na nje ya Bunge, inakinzani na msimamo wa awali wa mwanasiasa huyo juu ya kugombea muhula wa tatu wa urais.

Mwishoni mwa mwaka uliopita 2019, Rais Outtara alisema atawania tena urais kwa muhula wa tatu mfululizo endapo watangulizi wake pia wataamua kujitosa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi huo, na ambao unatajwa kama kipimo muhimu cha kutathmini uthabiti wa nchi hiyo baada ya kukumbwa na vita vya ndani mara mbili katika karne hii ya 21.

Kabla ya hapo, Outtara mwenye umri wa miaka 77 alitoa kauli nyingine ya kukinzana, ambapo alisema anakusudia kukabidhi madaraka kwa kizazi cha vijana na wakati huohuo akadai pia kwamba, mabadiliko ya katiba ya mwaka 2016 yaliondoa kikomo cha muhula wa urais na hivyo anaweza kuwania tena kwa mara ya tatu, wazo ambalo wapinzani wake walilipinga.

Rais wa zamani wa Kodivaa, Laurent Gbagbo katika mahakama ya ICC

Outarra alichaguliwa mara ya kwanza mwaka 2010, katika uchaguzi ulioibua ghasia za ndani baada ya mtangulizi wake Laurent Gabgbo kukatalia madarakani. Watu zaidi ya elfu tatu waliuawa katika machafuko hayo ya baada ya uchaguzi.

Uchaguzi wa rais wa Oktoba mwaka huu nchini Kodivaa unaonekana mgumu mno kutabiri hususan kutokana na ukweli kwamba, hasimu mkuu wa kisiasa Rais Outtara, Laurent Gbagbo anatazamiwa kurejea kwenye ulingo wa siasa kuwania kiti hicho, baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kumtoa hatiani kuhusiana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ya kutenda jinai dhidi ya binadamu.