UN yalaani mauaji ya wasichana na wanawake mjini Tripoli, Libya
Umoja wa Mataifa umelaani shambulizi la mabomu katika mji mkuu wa Libya Tripoli, ambalo liliua na kujeruhi watoto wa kike na wanawake kadhaa.
Katika ujumbe uliotumwa na UN kwenye ukurasa wake wa Twitter, umoja huo umesema waliouawa katika hujuma hiyo iliyoripotiwa na Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ni mabinti watano wenye umri wa miaka 14 hadi 20 huku wasichana watano akiwemo wa miaka 11 wakijeruhiwa vibaya.
Shambulizi hilo la juzi Jumatano kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli lilifanyika masaa machache baada ya kutolewa mwito na jamii ya kimataifa wa kutaka kusitishwa vita kwa muda kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya kirusi cha corona.
Kwa mujibu wa Amin Hashem, Mshauri wa Habari wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, miongoni mwa waliouawa ni watoto wa kike watatu wa familia moja baada ya kundi la wanamgambo linalojiita jeshi la kitaifa la Libya linaloongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar kulishambulia kwa mabomu eneo la Ain Zara na Bin Ghahsir kusini mwa Tripoli.
Hii si mara ya kwanza kwa wanamgambo wa Khalifa Haftar kushambulia eneo la makazi ya watu na kuua raia wasio na hatia, ingawaje mara zote wamekuwa wakikanusha kuhusika na hujuma hizo.
Tokea Aprili mwaka jana wakati Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji mkuu Tripoli, maelfu ya watu wakiwemo watoto wadogo na wanawake wameuawa na kujeruhiwa, mbali na wengine 150,000 kuachwa bila makao.