Corona, Sudan yaomba msaada wa matibabu kutoka China
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60394-corona_sudan_yaomba_msaada_wa_matibabu_kutoka_china
Serikali ya Sudan imeiomba serikali ya China iisaidie nchi hiyo dawa na vifaa vya matibabu kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2020 20:13 UTC
  • Corona, Sudan yaomba msaada wa matibabu kutoka China

Serikali ya Sudan imeiomba serikali ya China iisaidie nchi hiyo dawa na vifaa vya matibabu kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Televisheni ya 'Rusia al Yaum' jana Jumatano ilimnukuu Dk. al Sadiq Abdul Aziz, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan akiwasilisha ombi hilo rasmi wakati alipokutana na balozi wa China mjini Khartoum. 

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadiliana njia za kuzidisha ushirikiano baina yao, kieneo na kimataifa hususan katika masuala ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, balozi wa China amesema katika mazungumzo hayo kuwa nchi yake inayaelewa vizuri mazingira ya afya na matibabu yalivyo nchini Sudan na ameahidi kuwa Beijing itatuma misaada yake ya masuala ya tiba haraka iwezekanavyo huko Sudan.

Sudan ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuathiriwa na COVID-19 barani Afrika

 

Kabla ya hapo Sudan ilikuwa imeahidiwa na Umoja wa Ulaya kupewa msaada wa Euro milioni 80 kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya corona.

Serikali ya Sudan imetangaza marufuku ya kutotoka nje katika baadhi ya miji na maeneo ya nchi hiyo kama sehemu ya vita vya nchi nzima vya kupambana na uvonjwa wa COVID-19.

Hadi jana Jumatano idadi ya watu waliokuwa wamekumbwa na ugonjwa wa corona nchini Sudan ilikuwa imeshafikia 32, watano kati yao walikuwa wameshafariki dunia na wanne walikuwa wameshapata afueni na kuruhusiwa kutoka hospitalini.