Maelfu wapanga foleni kupewa kinywaji 'kinachotibu' corona Madagascar
Maelfu ya wananchi wa Madagascar jana Alkhamisi walionekana kwenye foleni ndefu za kupokea kile kinachotajwa kuwa kinywaji malumu cha asili, cha kutibu ugonjwa wa Covid-19 unaojulikana kwa jina maarufu la corona.
Kinywaji hicho cha asili kilizinduliwa rasmi mapema wiki hii na Rais Andry Rajoelina wa nchi hiyo, aliyedai kuwa tayari kimeshawatibu wagonjwa wawili wa Covid-19 nchini humo.
Rais wa kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa Afrika amesema, "majaribio yote yamefanywa na uwezo wake wa kupunguza dalili za ugonjwa huo umepasishwa. Dawa hii ya asili sasa imedhinishwa kutibu wagonjwa wa Covid-19 Madagascar."
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, maelfu ya wananchi wa Madagascar walipanga foleni ndefu wakisubiri kupewa kinywaji hicho cha asili cha 'kutibu" corona na maafisa wa serikali waliokuwa wamevalia barakoa.

Mwanamke mmoja aliyekuwepo kwenye foleni akisubiri kupewa kinywaji hicho ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "rais amesema kinywaji hiki kinaponya, tunakunywa kwa kuwa tunamuamini."
Katika ujumbe wake kwenye Twitter, Rais Andry Rajoelina wa Madagascar ameandika, "nimefanya mazungumzo ya kufana kwa njia ya video na Rais Tshisekedi wa DRC, ambaye ametupongeza kwa kuvumbua dawa hii ya kienyeji ya kutibu Covid-19."