Kampeni za uchaguzi mkuu kuanza kesho Jumatatu nchini Burundi
-
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ametia saini rasmi amri ya kuanza kampeni za uchaguzi mkuu wa rais bunge na madiwani nchini humo. Kampeni hizo zitaanza kesho Jumatatu na kuendelea hadi Jumapili ya tarehe 17 mwezi ujao wa Mei.
Katika kipindi hicho cha wiki tatu, kampeni za uchaguzi zitakuwa zinaanza saa 12 asubuhi na kumalizika saa 12 jioni kila siku. Ni marufuku kuendesha kampeni zozote nje ya muda huo na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo hayo.
Amri hiyo ya Rais wa Burundi aidha imesema, kampeni itabidi zifanywe na vyama vya siasa, miungano ya vyama vya siasa na wagombea binafsi walioidhinishwa na Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Baraza la Vyombo vya Habari vya Taifa litahakikisha kuwa wagombea wote wanapewa haki sawa za kujitangaza wakati wa kampeni.
Kampeni hizo za uchaguzi mkuu zinaanza kesho nchini Burundi wakati huu ambapo nchi hiyo imezungukwa na nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa COVID-19 maarufu kwa jina la corona ambao unaenea kwa kasi kwenye mikusanyiko ya watu.
Hadi leo mchana, nchi jirani ya Tanzania ilikuwa imethibitisha watu 299 wamekumbwa na ugonjwa huo, nchi nyingine jirani ya Rwanda ina wagonjwa 183 huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ikiwa imeshathibitisha kuwa na wagonjwa 442 wa corona hadi leo mchana.