Chama kikuu cha upinzani Zimbabwe chaitaka polisi ieleze waliko wanaharakati waliotoweka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60991-chama_kikuu_cha_upinzani_zimbabwe_chaitaka_polisi_ieleze_waliko_wanaharakati_waliotoweka
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Harakati kwa ajili ya Mabadiliko ya Kidemokrasia (MDC) kimesema, wanaharakati wake watatu wametoweka baada ya kushiriki maandamano ya kulalamikia uhaba wa chakula; na polisi inakana kuwashikilia wakati awali ilivieleza vyombo vya habari vya ndani kwamba wanaharakati hao walikuwa wamekamatwa.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 15, 2020 03:24 UTC
  • Chama kikuu cha upinzani Zimbabwe chaitaka polisi ieleze waliko wanaharakati waliotoweka

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Harakati kwa ajili ya Mabadiliko ya Kidemokrasia (MDC) kimesema, wanaharakati wake watatu wametoweka baada ya kushiriki maandamano ya kulalamikia uhaba wa chakula; na polisi inakana kuwashikilia wakati awali ilivieleza vyombo vya habari vya ndani kwamba wanaharakati hao walikuwa wamekamatwa.

Msemaji wa polisi Paul Nyathi alinukuliwa na vyombo rasmi vya habari vya serikali na vya binafsi akisema kuwa wanaharakati hao watatu walitiwa nguvuni kwa kushiriki maandamano yasiyo na kibali yaliyofanyika siku ya Jumatano.

Hata hivyo katika taarifa iliyotoa hapo jana, polisi ya Zimbabwe ilikanusha kuwa inawashikilia wanaharakati hao watatu wa chama cha MDC na kusema, vyombo vya usalama vinawatafuta watu hao ili kuwahoji kuhusiana na maandamano hayo yaliyoshirikisha makumi tu ya watu.

Maandamano ya upinzani, Zimbabwe

Kwa kuzingatia rekodi za kutoweka wapinzani wa serikali nchini Zimbabwe, MDC imesema, inahofia wanachama wake hao akiwemo mbunge mmoja watakuwa wametekwa nyara na maafisa wa usalama wa serikali.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimetoa taarifa ya kutaka wanachama wake hao waachiliwe huru haraka na bila ya masharti yoyote.

Kituo cha wanasheria kiitwacho Mawakili wa Zimbabwe kwa ajili ya Haki za Binadamu chenye makao yake katika mji mkuu wa nchi hiyo Harare kimesema kimewasilisha madai Mahakama Kuu kwa niaba ya familia za wanaharakati hao wa MDC kuitaka mahakama iibane polisi ili ieleze waliko watu hao.../