IGAD: Watu wasiopungua milioni 27 Afrika Mashariki wanakabiliwa na uhaba wa chakula
(last modified Fri, 05 Jun 2020 02:26:49 GMT )
Jun 05, 2020 02:26 UTC
  • IGAD: Watu wasiopungua milioni 27 Afrika Mashariki wanakabiliwa na uhaba wa chakula

Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD) limetangaza kuwa watu wasiopungua milioni 27.6 walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki mwaka jana, kabla ya kuibuka janga la COVID-19.

Ripoti kuhusu mgogoro wa cakula iliyotolewa na IGAD mjini Nairobi, Kenya imesema, watu hao wanahitaji msaada wa dharura.

Katibu Mkuu wa IGAD Workneh Gebeyehu amesema, kanda hiyo inakabiliwa na tishio la usalama wa chakula ambalo halijawahi kutokea kwa miongo kadhaa kutokana na hali mbaya inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na uvamizi wa nzige wa jangwani, na changamoto nyingine kubwa ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 au corona na mafuriko katika ardhi ya kilimo.

Hata hivyo, ripoti hiyo imesema janga la COVID-19 linaweza kuzidisha idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula kuliko makadirio hayo.

Mapigano ni moja ya sababu za kuenea njaa mashariki mwa Afrika

David Phiri, mratibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FA0) katika eneo la Mashariki mwa Afrika amesema sasa kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula katika eneo hili hilo.

Phiri ameonya kuwa, COVID-19, uvamizi wa nzige wa jangwani, mafuriko ya mara kwa mara na mapigano ni mambo ambayo yanahatarisha uwezo wa watu kupata chakula katika eneo hilo hilo.