Uturuki yasisitiza kushirikiana na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62006-uturuki_yasisitiza_kushirikiana_na_serikali_ya_muafaka_wa_kitaifa_libya
Waziri wa Ulinzi wa Uturuki ameutembelea mji mkuu wa Libya Tripoli, na kusema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 05, 2020 03:53 UTC
  • Uturuki yasisitiza kushirikiana na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya

Waziri wa Ulinzi wa Uturuki ameutembelea mji mkuu wa Libya Tripoli, na kusema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA).

Kwa mujibu wa taarifa, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar akiwa ameandamana na Mkuu wa Majeshi ya Uturuki Yasar Guler wamefika Tripoli na kufanya mazungumz na Fayez al-Sarraj, Rais wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya. Katika mkutano huo, Akar amesisitiza kuwa, Uturuki itaendelea kuwa pamoja na watu wa Libya na itachukua hatua zozote zinazohitajika kwa ajili ya kuwasaidia.

Taarifa ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya nayo imetangaza kuwa, katika mkutano wa Al Sarraj na Akar, pande mbili zimechunguza matukio ya hivi karibuni ya Libya na pia mpango wa kuimarisha jeshi la nchi hiyo katika fremu ya mapatano yaliyotiwa saini baina ya Uturuki na Libya.

Wakati huo huo Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema safari ya Akar mjini Tripoli imefanyika katika muendelezo wa jitihada za kuimarisha uhusiano wa nchi mbili. Erdogan amesema lengo kuu la safari yake mjini Doha, Qatar siku ya Alhamisi lilikuwa ni kujadili hali ya mambo Libya.

Rais Erdogan wa Uturuki (kulia) na Waziri Mkuu wa Libya Al-Sarraj

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Haftar anapata uungaji mkono wa kijeshi kutoka Umoja wa Falme za Kiarbau, Misri, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Ulaya.