Wasomi, wanachuo wa Kenya nchini Marekani wakosoa agizo la Trump dhidi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62139-wasomi_wanachuo_wa_kenya_nchini_marekani_wakosoa_agizo_la_trump_dhidi_yao
Wahadhiri na wanachuo raia wa Kenya walioko Marekani wamekosoa vikali agizo lililotolewa na rais wa nchi hiyo, Donald Trump, la kutaka wanafunzi wote wa kigeni waondoke nchini humo ndani ya miezi miwili ijayo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 11, 2020 10:18 UTC
  • Wasomi, wanachuo wa Kenya nchini Marekani wakosoa agizo la Trump dhidi yao

Wahadhiri na wanachuo raia wa Kenya walioko Marekani wamekosoa vikali agizo lililotolewa na rais wa nchi hiyo, Donald Trump, la kutaka wanafunzi wote wa kigeni waondoke nchini humo ndani ya miezi miwili ijayo.

Profesa Kefa Otiso, mhadhiri raia wa Kenya katika Chuo Kikuu cha Bowling Green State jimboni Ohio amelitaja agizo hilo la Trump kama adhabu kali inayokusudia kuumiza. Amefafanua kuwa, "hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha uvurugaji huo wa ghafla wa maisha ya Wakenya nchini Marekani."

Msomi huyo wa Kenya amesema sera za utawala wa Trump zilizo dhidi ya raia wa kigeni zinapaswa kuangaziwa, huku akiutaka ubalozi wa Kenya mjini Washington umwandikie barua ya malalamiko Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo juu ya kadhia hiyo.

Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Wasomi wa Kenya nchini Marekani, Jerono Rotich, kuna wanachuo zaidi ya elfu nne katika Vyuo Vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Marekani, katika mwaka wa masomo 2019/20.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Wanafunzi wa nchi mbali mbali walioko Marekani wamekosoa vikali mpango huo wa Trump wa kuwafukuza nchini humo ndani ya miezi miwili ijayo.

Trump amesema iwapo vyuo hivyo havitakuwa vimefunguliwa ndani ya miezi miwili ijayo na masomo yakaendelea kwa njia ya Intaneti, basi serikali yake itawafutia wanachuo hao vibali vya kuendelea kuweko nchini humo.