Rwanda yasikitishwa na mauaji ya askari wake Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) limeeleza kusikitishwa kwake na mauaji ya askari wa kulinda amani wa nchi hiyo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katika taarifa ya jana Jumatano, RDF imesema, "tumesikitishwa mno na kifo cha askari wa kulinda amani, raia wa Rwanda ambaye alikuwa anahudumu chini ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MUNISCA)."
Aidha Jeshi la Ulinzi la Rwanda limetoa mkono wa pole kwa familia ya askari huyo aliyeuawa katika shambulizi la hivi karibuni, akiwa katika mstari wa mbele wa kurejesha amani na uthabiti nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umelaani vikali hujuma hiyo iliyofanywa dhidi ya askari wake wa kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo mbali na kuuawa askari mmoja wa kulinda amani raia wa Rwanda, wengine wawili walijeruhiwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu zake za rambi rambi kwa familia ya askari aliyeuawa, na pia kwa watu na serikali ya Rwanda. Amesema mashambulizi dhidi ya askari wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuhesabiwa kuwa ni jinai za kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013 baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.
Kwa sasa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajitahidi kurejesha utulivu katika nchi hiyo ya kati kati mwa Afrika.