Marais wa Misri na Ufaransa wajadiliana mgogoro wa Libya
Marais wa Misri na Ufaransa wamefanya mazungumzo ya simu kuhusiana na mgogoro wa Libya.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amefanya mazungumzo ya simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na wamejadiliana kwa upana mgogoro wa Libya.
Katika mazungumzo hayo marais hao wawili mbali na kubadilishana mawazo kuhusu matukio na hali ya hivi sasa ya Libya wametilia mkazo pia wajibu wa kupunguzwa kadiri inavyowezekana kile walichokiita ni uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Libya. Ikumbukwe kuwa kwa uungaji mkono wao wa kila hali kwa jenerali muasi Khalifa Haftar, Misri na Ufaransa ni miongoni mwa waingiliaji wakubwa wa masuala ya ndani ya Libya.
Nchi hizo mbili aidha zimetilia mkazo udharura wa kuendelea kushauriana na kufanya kazi kwa pamoja katika mgogoro wa Libya.
Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya mara kwa mara imekuwa ikilalamikia jinsi madola ajinabi yanavyoingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo na kufanya vita viendelee bila kikomo.
Sasa hivi wakati Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa ikiwa iko mbioni kuanza operesheni za kuukomboa mji wa Sirte, Misri imetuma shehena kadhaa za kijeshi kwenda kumsaidia jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" mashariki mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mwezi Aprili 2019, Khalifa Haftar huku akiungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi hasa Ufaransa, alianzisha mashambulizi ya pande zote kwa tamaa ya kuuteka mji mkuu Tripoli na kuipindua Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa lakini ndoto hiyo imeshindwa kuaguka.