Mapinduzi ya Kijeshi nchini Mali na kujiuzulu Rais Keita
Mapinduzi ya kijeshi yalijiri nchini Mali Jumanne ambapo Rais Ibrahim Boubacar Keita na Waziri Mkuu wake, Boubou Cissé walikamatwa na wanajeshi waasi. Masaa machache baada ya kukamatwa, Rais Keita alijitokeza katika televisheni ya taifa na kutangaza kujiuzulu huku akisisitiza hataki kubakia kwake madarakani kuwe chanzo cha umwagikaji damu.
Makamanda wa kijeshi walioongoza mapinduzi hayo wamesema kuwa, kutakuwa na kipindi cha mpito ambacho kitakuwa ni muda unaokubalika kiakili kisha baada ya hapo kutaitishwa uchaguzi mkuu. Aidha wameunda Kamati ya Wokovu wa Kitaifa itakayoiongoza nchi hiyo huku wakisisitiza kuwa watafungamana na mikataba yote ya kimataifa. Kanali Assimi Goita ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ya wokovu ya kitaifa ambayo itasimamia nchi hiyo katika kipindi cha mpito.
Mapinduzi ya sasa ya kijeshi nchini Mali yanajiri wakati ambao nchi hiyo mwaka 2012 pia ilishuhudia mapinduzi mengine ya kijeshi ambayo bado athari zake zinahisika. Kwa hakika mgogoro wa sasa wa Mali ulianza mwaka 2012 baada ya mapinduzi ya kijeshi wakati huo. Baada ya mapinduzi hayo, magaidi na wanagambo walizidisha hujuma zao katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Tokea wakati huo kumekuwepo na mazungumzo baina ya serikali na makundi mbali mbali ya wangambo kwa lengo la kurejesha utulivu nchini humo. Mazungumzo hayo hatimaye yalizaa matunda na kukatiwa saini mapatano ya amani mwaka 2015 baina ya serikali ya Mali na makundi ya upinzani. Mapatano hayo yalilenga kurejesha amani na kuhitimisha mashambulizi ya makundi ya wanamgambo. Lakini serikali ya Mali na wanamgambo, wote hawajafungamana na mapatano hayo na hivyo nchi hiyo bado haina utulivu. Aidha uwepo wa makundi ya kigaidi katika baadhi ya maeneo ya Mali ni chanzo cha ukosefu mkubwa wa usalama nchini humo.
Ukosefu wa usalama ni moja ya sababu kuu za wananchi kutoridhika na serikali ya nchi hiyo. Hali kadhalika kwa miaka kadhaa sasa nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa katika uga wa kisiasa na kiuchumi.
Keita alishindwa kutumiza ahadi zake za kiuchumi hasa katika uga wa kubuni nafasi za ajira na kuboresha maisha ya wananchi. Aidha kuibuka janga la corona na mgomo wa waalimu ni mambo mengine ambayo yamepelekea hali kuwa mbaya nchini Mali. Kwa hivyo hali mbaya ya kiuchumi pamoja na madai ya kuwepo wizi wa kura katika uchaguzi wa bunge wa mwezi Machi ni mambo ambayo yalipelekea wananchi wenye hasira kujitokeza mitaani na kuandamana dhidi ya serikali. Takwa kuu la waandamanaji limekuwa ni kumtaka Rais Keita ajiuzulu.
Nouhoum Togo msemaji wa Muungano wa MF-REP, ambao unawaleta pamoja viongozi wa kisiasa na kidini' amesema Keita hakuwa anataka kusikiliza matakwa ya wananchi. Anaongeza kuwa muungano huo hata ulimpa Keita pendekezo la mtu atakayechukua nafasi yake lakini alijibu pendekezo hilo kwa kuwaua waandamanaji.
Pamoja na kuwepo matatizo ya ndani ya nchi lakini uingiliaji wa kigeni nao pia imechangia katika matatizo ya Mali.
Katika miaka ya hivi karibuni, Ufaransa imetuma idadi kubwa ya wanajeshi wake nchini Mali kwa kisingizio cha kurejesha amani na utulivu nchini humo lakini ni wazi kuwa ina malengo ya ukoloni mambo leo. Mali ni nchi yenye utajiri mkubwa wa mali asili hasa madini ya urani, dhahabu, na pia hifadhi ya gesi na mafuta na hivyo Ufaransa inaikodolea macho ya tamaa nchi hiyo.
Ufaransa inalitazama kwa umuhimu mkubwa suala la kudhibiti vyanzo vya madini ya urani nchini Mali kwa sababu asilimia 78 ya nishati ya umeme ya Ufaransa hutegemea vituo vya nyuklia ambavyo navyo hutegemea madini ya urani na Mali ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa ya madini hayo.
Ni kwa msingi huo ndio katika miaka ya hivi karibuni Mali imegeuka na kuwa kituo muhimu kwa Ufaransa kwa ajili ya uwepo wake katika nchi zingine za Afrika. Katika safari yake nchini Mali, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliahidi kuunda kikosi maalumu cha kijeshi cha kukabiliana na makundi ya kigaidi na wanamgambo katika eneo la Afrika Magharibi. Kwa msingi huo, Ufaransa inatumia kisingizio cha kupambana na magaidi kuimarisha satwa yake nchini Mali na eneo zima la Afrika Magharibi.
Saeed Jaafar Qanadboshi, mtaalamu wa masuala ya Afrika anasema hivi kuhusu nukta hii. "Rais wa Mali alichaguliwa kwa kura za wananchi karibu miaka miwili iliyopita na uchaguzi wa bunge ulifanyika Mwezi Machi. Ni wazi kuwa kulikuwa na wizi mkubwa wa kura katika uchaguzi na hivyo serikali ilikosolewa vikali lakini ilipuuza ukosaji huo. Baada ya uchaguzi huo wananchi walijawa na hasara kwani wanaamini kuwa viongozi wa Mali ni vibaraka wa Ufaransa na kuwepo kwa wanajeshi 4,500 wa Ufaransa nchini humo ni sawa na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo."
Ufaransa imepinga vikali mapinduzi ya kijeshi nchini Mali na imeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama. Ni wazi kuwa kukaririwa uzoefu wa mwaka 2012 si jambo wanalotaka wananchi wa Mali au nchi za eneo. Kuibuka mgogoro wa kisiasa na ukosefu wa usalama Mali kunaweza kutoa mwanya ka makundi ya kigaidi kujiimarisha zaidi katika eneo.
Hali nchini Mali si shwari na kuendelea mgogoro nchini humo kunaweza kuvuruga uthabiti wa nchi jirani. Kwa hivyo uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa na kutekelezwa matakwa ya wananchi kunaweza kurejesha utulivu katika nchi hiyo. Hakuna shaka kuwa, kuendelea mgogoro nchini Mali kunaweza kuongeza hatari ya uingiliaji zaidi wa kigeni hasa wa Ufaransa katika nchi hiyo na eneo zima la magharibi mwa Afrika.