Ecowas yalitaka jeshi la Mali limtangaze rais ndani ya wiki moja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63288-ecowas_yalitaka_jeshi_la_mali_limtangaze_rais_ndani_ya_wiki_moja
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) imewataka wanajeshi wafanya mapinduzi huko Mali kumtangaza rais mpya wa mpito wa nchi hiyo kufikia Septemba 15.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2020 23:03 UTC
  • Ecowas yalitaka jeshi la Mali limtangaze rais ndani ya wiki moja

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) imewataka wanajeshi wafanya mapinduzi huko Mali kumtangaza rais mpya wa mpito wa nchi hiyo kufikia Septemba 15.

Taarifa iliyotolewa na Ecowas baada ya kikao cha jana Jumatatu imesisitiza kuwa, Rais na Waziri Mkuu wa mpito wa Mali watakaotangazwa katika kipindi cha wiki moja ijayo sharti wawe ni raia.

Kadhalika jumuiya hiyo ya kikanda yenye nchi wanachama 15 imebainisha kuwa, vikwazo ilivyotangaza dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi vitaendelea kuwepo hadi pale viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali watakapokabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia.

Kabla ya kikao cha jana, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger ambaye ni Mwenyekiti wa hivi sasa wa Ecowas alisema iwapo wanajeshi hao wafanya mapinduzi wataafiki pendekezo hilo la kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito, basi jumuiya hiyo ya kikanda itawafutia vikwazo ilivyotangaza, hatua kwa hatua.

Rais wa Mali aliyepinduliwa Ibrahim Boubacar Keita

Makanali kadhaa wa kijeshi wanaoliongoza taifa hilo tokea Agosti 18 baada ya kupinduliwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita, wamekuwa wakisisitiza kuwa wanapaswa kusalia madarakani kwa muda wa miaka mitatu ya kipindi cha mpito.

Keita hivi sasa yuko katika Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya matibabu baada ya hali yake ya afya kuzorota, huku mazungumzo ya kurejesha serikali ya kiraia nchini humo baada ya kipindi cha mpito kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyojiri mwezi uliopita yakikosa natija.