Rais Touadéra achaguliwa tena kuiongoza Jamhuri ya Afrika ya Kati
Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amechaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi kingine cha pili cha miaka mitano baada ya kutangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 27 Desemba.
Tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati jana ilimtangaza rais Touadéra mshindi wa uchaguzi wa rais baada ya kupata zaidi ya asilimia 53 ya kura zote.
Mwenyekiti wa tume hiyo Mathias Morouba ameeleza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika mji mkuu Bangui kwamba, Rais Faustin-Archange Touadéra anatangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa rais baada ya kunyakua asilimia 53.9 ya kura zote katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo.
Uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati uliandamwa na hujuma zilizoratibiwa za makundi ya waasi yaliyodhamiria kuvuruga zoezi la upigaji kura baada ya mahakama ya juu kabisa ya nchi hiyo kumzuia aliyekuwa rais wa nchi hiyo Francois Bozize kugombea katika uchaguzi huo.
Zoezi la upigaji kura lilikwama katika miji kadhaa kutokana na mashambulio na uharibifu wa vifaa vya kupigia kura uliofanywa katika siku tofauti ikiwemo ya uchaguzi wenyewe.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, karibu nusu ya waliotimiza masharti ya upigaji kura, yaani watu 910,000 walijiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Desemba 27 na takriban asilimia 76.3 miongoni mwao walishiriki katika upigaji kura.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2016 hadi sasa Rais Faustin-Archange Touadéra amekuwa akifanya jitihada kuhakikisha maeneo mengi makubwa ya nchi hiyo yanayoshikiliwa na makundi ya wanamgambo yanarejea kwenye udhibiti wa serikali.../