Wafaransa waua raia 20 waliokuwa harusini nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65620-wafaransa_waua_raia_20_waliokuwa_harusini_nchini_mali
Duru moja ya matibabu nchini Mali imetangaza kuwa, wanajeshi wa Ufaransa wameshambulia sherehe za harusi katika eneo moja la jangwani, katikati ya Mali na kuua zaidi ya raia 20 baadhi yao wakiwa ni watoto wadogo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2021 09:05 UTC
  • Wafaransa waua raia 20 waliokuwa harusini nchini Mali

Duru moja ya matibabu nchini Mali imetangaza kuwa, wanajeshi wa Ufaransa wameshambulia sherehe za harusi katika eneo moja la jangwani, katikati ya Mali na kuua zaidi ya raia 20 baadhi yao wakiwa ni watoto wadogo.

Shirika la habari la IRIB limeinukuu duru hiyo ikithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, mauaji hao yalitokea siku ya Jumapili. Duru hiyo imesema, wanajeshi wa Ufaransa walishambulia wapanda pikipiki katika vijiji vya Bounti na Kikara kwa kudhani kuwa ni magaidi. Hata hivyo wanajeshi wa Ufaransa waliwashambulia raia waliokuwa wamekusanyika kwenye sherehe za harusi na kuua zaidi ya 20 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.

Jeshi la Ufaransa limedai kuwa limeua makumi ya magaidi katika shambulio lake la anga katika eneo la Douentza, lililoko umbali wa kilomita 90 magharibi mwa mji wa Hambori katikati ya Mali.

Hata hivyo wanavijiji wa kijiji cha Bounti wamesema kuwa, helikopta moja ya Ufaransa ilifanya mashambulizi makubwa mchana kweupe dhidi ya mkusanyiko wa raia hao waliokuweko harusini na kusababisha hofu kubwa. 

Wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali

 

Mmoja wa waliokoka kwenye shambulizi hhilo la jeshi la Ufaransa aliyejitambulisha kwa jina la Ahmadou Ghana amesema, ilikuwa ni patashika, ilikuwa ni kila mmoja kukimbilia kuokoa maisha yake.

Mwanakijiji mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Mady Dicko amesema, tulifanyiwa shambulio kubwa na la kushtukiza la anga. Helikopta ya Ufaransa iliyotushambulia ilikuwa inaruka umbali wa chini kabisa kutoka angani.

Mali imo kwenye machafuko tangu mwaka 2012 baada ya wanajeshi kufanya mapinduzi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wa Ufaransa wako nchini humo tangu mwaka 2013 lakini kila leo raia wasio na hatia wanauawa kiholela.