Feb 20, 2021 03:10 UTC
  • WHO  yaanza kutoa chanjo ya Ebola DRC

Shirika la Afya Duniani WHO limeanza zoezi la kutoa chanjo ya Ebola ili kukabiliana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo nchini Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza Ijumaa, kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brazzaville Jamhuri ya Kongo, mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema juhudi hizo ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa, watu waliokutana nao, upimaji, matibabu pamoja na maandalizi ya chanjo. 

“Tunajitahidi sana na tunakwenda mbio kudhibiti virusi hivyo. Tukiwa na wataalamu na vifaa tayari mashinani , ni mwanzo mzuri”, amesema Dkt. Moeti.

Nchini Guinea ndege ya misaada ya kibinadamu imewasili Nzerekore Ijumaa hii ikiwa na shehena ya zaidi ya kilo 700 za vifaa tiba vilivyotolewa na WHO na washirika wake. 

Aidha zaidi ya dozi 11,000 za chanjo dhidi ya Ebola zinatarajiwa kuwasili nchini humo  Jumapili ya tarehe 21  Februari wiki hii. 

Kwa upande wake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC imeripoti wagonjwa wanne waliothibitishwa kuwa na Ebola ikiwemo vifo viwili. 

Mashariki mwa nchi hiyo WHO ina takriban wataalamu 20 ambao wanazisaidia mamlaka za afya za taifa na kikanda. 

Takriban dozi 8,000 za chanjo bado zilikuwepo nchini humo wakati ulipomalizika mlipuko wa 11 wa Ebola. 

Chanjo kwa watu ambao wako katika hatari kubwa zaidi ilizinduliwa rasmi Februari 15 Butembo Mashariki mwa DRC ambako ndio kitovu cha mlipuko wa sasa. 

Hadi kufikia Ijumaa  karibu watu 70 wameshapatiwa chanjo DRC.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.

Tags