UN: Vikwazo vya silaha dhidi ya Libya havina athari yoyote
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67984-un_vikwazo_vya_silaha_dhidi_ya_libya_havina_athari_yoyote
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema vikwazo vya silaha vya umoja huo dhidi ya Libya vinaendelea kukiukwa na kwa msingi huo havina taathira yoyote.
(last modified 2026-02-23T08:13:53+00:00 )
Mar 17, 2021 07:31 UTC
  • UN: Vikwazo vya silaha dhidi ya Libya havina athari yoyote

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema vikwazo vya silaha vya umoja huo dhidi ya Libya vinaendelea kukiukwa na kwa msingi huo havina taathira yoyote.

Katika taarifa yao jana Jumanne, watalaamu hao wa Umoja wa Mataifa walisema: Nchi ajinabi zinazorundika silaha Libya na walezi wa mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika zikiwemo nchi Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Uturuki zinadhibiti mnyororo wa kupelekwa silaha Libya, na hivyo kutia ugumu katika uchunguzi wa wataalamu hao.

Taarifa hiyo ya wataalamu wa UN imesema nchi hizo vamizi zinaendelea kuchochea mgogoro Libya kwa kuyaunga mkono moja kwa moja makundi hasimu; huku zikipuuza vikwazo hivyo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.

Hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa mwito wa kuondoka mara moja kutoka nchini Libya majeshi yote ya kigeni na mamluki wanaoendesha mapigano katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika; sanjari na kuzitaka nchi wanachama wa baraza hilo kuheshimu vikwazo vya silaha vya UN dhidi ya Libya.

Wanajeshi wa Uturuki na magari yao ya deraya nchini Libya

Libya iliwekewa vikwazo vya silaha na Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2011, hata hivyo baadhi ya mataifa ikiwemo Imarati na Uturuki mara kadhaa yamekiuka vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya muda ya Umoja wa Kitaifa ya Libya iliapishwa juzi Jumatatu na kuanza rasmi shughuli zake. Jumatano iliyopita, Bunge la Libya lililipigia kura Baraza la Mawaziri la nchi hiyo na kulipasisha kwa wingi mutlaki yaani kwa kura 132 kati ya 133 za wabunge waliohudhuria kikao hicho.