Wahajiri 130 wahofiwa kufariki dunia baada ya mtumbwi wao kuzama nchini Libya
Taarifa kutoka nchini Libya zinasema kuwa, mtumbwi mmoja uliokuwa umebeba watu 130 umezama karibu na fukwe za nchi hiyo.
Vyombo vya habari vimewanukuu maafisa wa misaada wa Libya wakitangaza kuwa, baada ya kutumwa katika eneo la tukio, wamefanikiwa kuopoa miili 10 ya wahajiri iliyokuwa inaelea juu ya maji, na kwamba hadi wanaripoti habari hiyo hakukuwa na mtu yeyote aliyepatikana hai.
Kabla ya hapo, shirika la kimataifa la wahajiri lilikuwa limetoa ripoti na kusema kuwa, wakimbizi 1,200 walipoteza maisha mwaka jana 2020 wakati walipojaribu kusafiri kwa njia ya baharini kinyume cha sheria, katika bahari ya Mediterranean kuelekea barani Ulaya.
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia imesema kuwa, katika kipindi cha miezi miwili ya mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021, idadi ya wahajiri walioingia kwenye fukwe za nchi hiyo ya Ulaya kwa kutumia bahari ya Mediterranean, iliongezeka.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Machi, karibu wahajiri 100 jana waliokolewa katika fukwe za magharibi mwa Libya wakati walipojaribu kusafiri kwa boti dhaifu kuelekea barani Ulaya. 20 kati yao walikufa maji.
Watu wanaoendesha magendo ya wanadamu wanatumia vibaya mwanya wa kukosekana serikali kuu huko Libya tangu baada ya kupinduliwa Muammar Gaddaf mwaka 2011, kupitishia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wahajiri wanaokimbilia maisha bora barani Ulaya kama wanavyojidanganya.
Kikosi cha gadi ya ufukweni cha Libya kimewaokoa wahajiri wengi ambao sehemu yao kubwa ni kutoka nchi za barani Afrika, waliojaribu kuvuka bahari kwa kutumia mitumbwi kuelekea Italia. Wahajiri hao sasa hivi wamepelekwa mjini Tripoli Libya na wamekabidhiwa kwa Taasisi ya Kimataifa ya Wahijri (IOM)