Bunge la Nigeria lataka kushughulikiwa tatizo la ukosefu wa usalama unaoikabili nchi
Bunge la Nigeria limepasisha maazimio kadhaa yanayomtaka Rais wa nchi, vikosi vya ulinzi na jeshi la polisi nchini humo kushughulikia tatizo la ukosefu wa usalama katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo ambalo limekuwa likiyatesa maeneo hayo kwa miaka kadhaa sasa.
Maazimio hayo yanamtaka Rais Muhamadu Buhari atangaze haraka hali ya hatari kuhusiana na mgogoro na tatizo la ukosefu wa usalama na amani ili kuchukuliwe hatua zote madhubuti za kudhamini tena amani na usalama wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Maazimio hayo yamepasishwa katika hali ambayo, Nigeria kwa muda sasa imekuwa ikiandamwa na wimbi la vitendo vya utumiaji mabavu na ukiukaji wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na hivyo kuikwamisha pakubwa nchi hiyo inayohesabiwa kuwa na uchumi mkubwa barani Afrika.
Vikosi vya usalama vilivyopelekwa katika majimbo mengi ya Nigeria kwa ajili ya kurejesha na kusimamia usalama, havina ubavu wa kukabiliana na wimbi la mashambulio yanayotekelezwa na makundi ya wabeba silaha likiwemo la Boko Haram.

Kaskazini magharibi mwa Nigeria hali ni mbaya ambapo kumekuwa kukishuhudiwa mara kwa mara vitendo vya kutekwa nyara mamia ya watoto wa shule.
Aidha eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo hali ni mbaya zaidi ambapo kwa zaidi ya muongo mmoja sasa vikosi vya usalama vimekuwa vikiendesha vita dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria ameendelea kukosolewa kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kuliangamiza kundi hilo la kigaidi ambalo limekuwa mara kwa mara likiteka nyara pia mamia ya wanafunzi na hata kuwatumia vijana wadogo kama askari vitani.