Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya akutana na Rais wa Tunisia
Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya amehimiza kurahishishwa mawailiano na sekta ya uchukuzi baina ya nchi yake na Tunisia.
Hayo yameripotiwa na gazeti la al Quds al Arabi ambalo limemnukuu Mohamed al-Menfi, Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya akisema hayo mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu Carthage nchini Tunisia baada ya kuonana na Rais Kais Said wa nchi hiyo.
Menfi ameongeza kuwa, katika mazungumzo yake na Rais wa Tunisia, pande mbili zimetilia mkazo wajibu wa kutatuliwa matatizo ya raia wa Tunisia na Libya wanaoingia kwenye nchi hizo mbili kama ambavyo zimehimiza pia wajibu wa kurahisishwa njia za kuingiza na kutoa bidhaa katika mipaka ya nchi hizo mbili jirani.
Mkuu huyo wa Baraza la Uongozi la Libya vile vile amesema, upande wa usalama pia ni miongoni mwa masuala muhimu aliyoyajadili na Rais wa Tunisia na pande zote mbili zimehimiza mno wajibu wa kulindwa utulivu na usalama katika eneo hilo.
Amesema, usalama wa Libya ni usalama wa Tunisia kama ambavyo usalama na utulivu wa Tunisia pia ni usalama na utulivu wa Libya na ameelezea matumaini yake kwamba safari za kutembeleana viongozi wa nchi mbili na ushirikiano baina yao utadumisha amani na utulivu katika nchi hizo na eneo hilo zima kiujumla.
Kwa upande wake Rais Kais Said wa Tunisia amesema kwenye mazungumzo hayo na wandishi wa habari kwamba Tunis ina nia ya kweli ya kuimarisha uhusiano wake na Tripoli katika nyuga zote hasa za kiuchumi na kiusalama.
Mohamed al-Menfi aliwasili nchini Tunisia juzi Jumamosi na safari yake hiyo rasmi ya siku tatu, inamalizika leo Jumatatu.