Sisitizo la Macron kuhusu kusitishwa uingiliaji wa kigeni nchini Libya
-
Emmanuel Macron
Katika hali ambayo kunafanyika jitihada za kuhitimisha mgogoro wa Libya ili uchaguzi utakaoyashirikisha makundi yote ya kisiasa ufanyike, uwepo wa wanajeshi wa kigeni na uingiliaji wa madola ajinabi katika mchakato wa amani nchini humo vinatambuliwa kuwa ni kizuizi katika kufikia amani ya kudumu.
Kuhusiana na nukta hiyo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Libya, Abdul Hamid Dbeibah mjini Paris Juni Mosi alisisitiza udharura wa kuondoka wanajeshi wa kigeni nchini humo.
Sisitizo la Macron la madola ya kigeni kuacha kuingilia mambo ya ndani ya Libya linatolewa katika hali ambayo Ufaranysa yenyewe ni miongoni mwa wahusika wakuu katika kuibua mgogoro wa sasa katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.
Kwa muongo mmoja sasa madola ya kikanda na ya nje ya eneo hilo yamekuwa yakiingilia mambo ya ndani ya Libya na kuisababishia nchi hiyo matatizo makubwa ambayo yangali yanaendelea kushuhudiwa. Sababu ya madola ajinabi kuingilia mambo ya ndani ya Libya na kutaka kuwa na ushawishi nchini humo ni utajiri mkubwa wa mafuta na gesi nchini humo. Sababu nyingine ni nafasi muhimu ya kistratijia ya Libya nchi ambayo imepewa lakabu ya "paa la Afrika". Aidha Katika Bahari ya Mediterranea, Libya inapakana na nchi muhimu za Ulaya. Ni kutokana na nukta hizo ndio maana madola makubwa yakawa yanaikodolea macho ya tamaa Libya.
Wakuu wa Ufaransa wamekuwa wakifuatilia kwa karibu matukio ya Libya na wameonyesha radimalia yao kuhusiana na yanayojiri nchini humo. Kwa mfano Ufaransa imekuwa ikikosoa wazi wazi hatua ya Uturuki kutuma askari wake Tripoli kwa ajili ya kuiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.
Hivyo ni wazi kuwa Ufaransa ina malengo ya muda mrefu katika kuingilia mambo ya ndani ya Libya na moja ya malengo hayo ni kutaka kushirikishwa zaidi katika miradi ya uzalishaji mafuta ya petroli nchini humo na pia kuwa na ushawishi jumla katika uchumi wa Libya na eneo zima la Afrika Kaskazini. Kilichowazi ni kuwa Ufaransa inaeneza satwa yake ya ukoloni mambo leo nchini Libya na katika eneo zima la Afrika Kaskazini na inatumia visingizio mbalimbali vya kiuchumi, kisiasa na kiusalama kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo.
Kuhusiana na nukta hiyo, Libya sasa inahesabiwa kuwa lango la kujipenyeza Ufaransa katika eneo zima la Afrika Kaskazini na pia katika nchi za Ukanda wa Sahel barani Afrika. Nchi za eneo hilo zina umuhimu mkubwa sana wa kiuchumi na kiusalama kwa Paris.
Hivi sasa kuna idadi kubwa ya wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali na nchi zingine za Ukanda wa Sahel na hii inatokana na kuwa, nchi hizo zinakidhi mahitaji muhimu ya kiuchumi ya Ufaransa hasa madini ya urani ambayo yanatumika kudhamini asilimia kubwa ya umeme wa Ufaransa.

Weledi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa, maslahi ya Ufaransa katika eneo hilo la Afrika ni ya kiuchumi na inatumia jeshi lake kulinda maslahi hayo hasa mafuta ghafi ya petroli na madini ya urani. Inakadiriwa kuwa asilimia 75 ya umeme wa Ufaransa inazalishwa kutokana na madini ya urani ambayo yanachimbwa barani Afrika.
Katika hali ya hivi sasa, ingawa wakuu wa Ufaransa wanadai kuwa wanaunga mkono mchakato wa kurejesha amani nchini Libya lakini ukweli ni kuwa, wanafuatilia maslahi ya kiuchumi na wanataka kuendelea kuwa na ushawishi katika nchi hiyo bila kuwa na washindani wenye nguvu.
Kwa hivyo sisitizo la hivi karibuni la Macron la kutaka askari wa kigeni waondoke Libya na kusitishwa uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo litakubalika tu iwpao Ufaransa yenyewe itawaacha Walibya wenyewe wajiamulie mambo na mustakabali wa nchi yao.