Mahakama ya Katiba Comoro yaidhinisha ushindi wa Kamanda Azali Assoumani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7144-mahakama_ya_katiba_comoro_yaidhinisha_ushindi_wa_kamanda_azali_assoumani
Mahakama ya Katiba nchini Comoro imemtangaza Kamanda Azali Assoumani kuwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais katika visiwa hivyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 15, 2016 23:08 UTC
  • Mahakama ya Katiba Comoro yaidhinisha ushindi wa Kamanda Azali Assoumani

Mahakama ya Katiba nchini Comoro imemtangaza Kamanda Azali Assoumani kuwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais katika visiwa hivyo.

Akiongea jana Jumapili katika mji mkuu Moroni, Lutfi Soulamaine, Rais wa Mahakama ya Katiba nchini humo amesema kuwa Assoumani ndiye mshindi halali wa kiti hicho baada ya kupata asilimia 41.43 ya kura halali zilizopigwa na kumbwaga hasimu wake wa karibu, Makamu wa Rais Mohamed Ali Soilihi, aliyewania kiti hicho kupitia chama tawala na kujizolea asilimia 39.6 ya kura hizo. Mouigni Baraka, Gavana wa kisiwa cha Grande Comore ameibuka wa tatu kwa kujikusanyia asilimia 18.9 ya kura.

Mahakama ya Katiba nchini Comoro ilitoa amri ya kurudiwa uchaguzi katika maeneo 13 ya nchi hiyo ya visiwa kutokana na dosari zilizojitokeza katika uchaguzi wa tarehe 10 mwezi uliopita wa Aprili.

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, Kamanda Azali Assoumani, anayeungwa mkono na Ahmed Abdallah Mohamed Sambi, rais wa zamani wa nchi hiyo alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 40.98 ya kura na hivyo kumshinda mpinzani wake Mohamed Ali Soilihi mgombea wa chama tawala aliyepata asilimia 39.87 ya kura.

Kamanda Azali Assoumani ni mmoja wa makamanda wa zamani wa jeshi na aliyewahi kuendesha mapinduzi ya kijeshi nchini humo. Kadhalika alikuwa rais wa visiwa vya Comoro kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2002 na kuanzia 2002 hadi 2006.