Ghannouchi: Imarati imeunga mkono na kufadhili mapinduzi baridi ya Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73022-ghannouchi_imarati_imeunga_mkono_na_kufadhili_mapinduzi_baridi_ya_tunisia
Rached Ghannouchi Spika wa Bunge lililosimamishwa la Tunisia amesema kuwa Imarati imefadhili mapinduzi yaliyotokea nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2021 05:38 UTC
  • Ghannouchi: Imarati imeunga mkono na kufadhili mapinduzi baridi ya Tunisia

Rached Ghannouchi Spika wa Bunge lililosimamishwa la Tunisia amesema kuwa Imarati imefadhili mapinduzi yaliyotokea nchini humo.

Rached Ghannouchi ameashiria taarifa ya Imarati iliyounga mkono uamuzi was Rais Kais Saeid wa Tunisia wa kumfukuza Waziri Mkuu na kusitisha shughuli za Bunge na kushika madaraka yote ya nchi na kusema: Imarati inavitambua vyama vya Kiislamu kuwa ni tishio kwa mipango yake ya kupanua ushawishi na satua yake na imechukua uamuzi wa kuzima mapinduzi ya Kiirabu katika nchi yalipoanzia yaani Tunisia. 

Ghannouchi ametahadharisha kwamba, kuna uwezekano wa kupamba moto malalamiko ya wananchi mitaani iwapo Rais Kais Saeid hatatengua uamuzi wake wa kusitisha shughuli za Bunge.

Baada ya kusimamisha shughuli za Bunge na kumtimua Waziri Mkuu, Hichem Mechichi Jumapili iliyopita, na vilevile kuwafukuza mawaziri wa ulinzi na sheria siku moja baadaye, Saied ameamuru kufutwa kazi maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa serikali ya Tunis.

Rais Kais Saeid wa Tunisia

Rais huyo wa Tunisia mwenye umri wa miaka 63, vilevile ametoa amri ya kufukuzwa orodha ndefu ya maafisa wakuu wa serikali, pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jeshi.

Vilevile ameondoa kinga ya wabunge na kuchukua mamlaka ya kimahakama. Aidha ameamuru kufanyika uchunguzi dhidi ya vyama vitatu vya kisiasa kwa tuhuma za kupokea fedha kutoka nje ya nchi kabla ya uchaguzi wa 2019.

Maamuzi hayo ya Rais Kais Saied wa Tunisia yamepingwa vikali na vyama vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya siasa.