Ennahdha yakadhibisha habari ya kukamatwa kinara wake, Rached Ghannouchi
Chama cha Ennahdha kimekadhibisha habari inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa kiongozi wa chama hicho Rached Ghannouchi ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tunisia amewekwa kwenye kifungo cha nyumbani.
Riyad al-Suaybi ambaye ni naibu wa Rached Ghannouchi amekadhibisha habari hiyo na kusema habari zinaochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Spika wa Bunge na kiongozi wa chama cha Ennahdha amewekwa kwenye kifungo cha nyumbani hazina ukweli wowote.
Awali shirika la habari la Reuters lilikuwa limeripoti kuwa, Rached Ghannouchi amehamishiwa kwenye hospitali ya kijeshi. Hata hivyo ripoti hiyo haikueleza sababu ya kulazwa hospitalini kiongozi huyo wa chama cha Ennahdha.
Rais Kais Saeid wa Tunisia tarehe 25 mwezi Julai mwaka huu alimfuta kazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hicham Mechichi na kisha akasimamisah shughuli zaBunge akisema amechukua hatua hiyo katika juhudi za kurejesha amani na uthabiti nchini Tunisia.
Wapinzani wake wameitafsiri hatua hiyo kuwa ni mapinduzi baridi aliyofanya kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo.
Spika wa Bunge la Tunisia, Rached Ghannouchi amesema hatua aliyochukua Rais Kais Saied ni mapinduzi dhidi ya mapinduzi ya wananchi, katiba ya nchi na uhuru wa taifa.
Hadi sasa miito mbalimbali imetolewa na ingali inaendelea kutolewa kieneo na kimataifa ya kutaka mgogoro na taharuki hiyo ya kisiasa iliyotokea Tunisia itatuliwe kwa njia ya mazungumzo na kuzuia kuitumbukiza nchi hiyo ya kaskazini katika vurugu na machafuko.