Wahajiri kadhaa wakiwemo watoto waaga dunia kwa kiu Tunisia
Wahajiri wapatao sita wakiwemo watoto wadogo wanne wamefariki dunia kwa kiu katika Jangwa la Sahara nchini Tunisia, mpakani mwa nchi hiyo na Algeria.
Aymen Béjaoui, Gavana wa eneo la Tozeur nchini Tunisia amenukuliwa na vyombo vya habari akisema hayo na kuongeza kuwa, akhthari ya wahajiri hao waliopoteza maisha ni raia kutoka nchi za eneo la Chini ya Jangwa la Sahara.
Ameongeza kuwa, wahamiaji hao waliaga dunia baada ya kukumbwa na kiu kali katika Jangwa Sahara ambalo linashuhudia kiwango cha juu cha joto. Kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa ya Tunisia, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika juzi Jumatano ilisajili nyuzijoto 50.
Habari zaidi zinasema kuwa, wahajiri hao walitembea kilomita kadhaa kabla ya kukumbana na mauti kutokana na kiu kali, wakiwa na azma ya kufika katika Bahari ya Mediterania kwa lengo la kutafuta njia za kuelekea barani Ulaya kupitia usafiri wa boti.
Katika wiki za hivi karibuni, wapiga mbizi na timu za waokoaji nchini Tunisia wameopoa makumi ya maiti za wahajiri waliozama baharini wakiwa katika safari hatarishi za kuelekea Ulaya.
Aghalabu ya wahajiri hao haramu ambao kutokana na sababu za kiuchumi huamua kuziacha nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, wanatokea katika nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia.