Rais wa Tunisia arefusha muda wa kusimamishwa shughuli za Bunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73866-rais_wa_tunisia_arefusha_muda_wa_kusimamishwa_shughuli_za_bunge
Rais wa Tunisia Kais Saied ametangaza kuwa, shughuli za Bunge la nchi hiyo zitaendelea kusitishwa kwa muda usiojulikana.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Aug 24, 2021 03:15 UTC
  • Rais wa Tunisia arefusha muda wa kusimamishwa shughuli za Bunge

Rais wa Tunisia Kais Saied ametangaza kuwa, shughuli za Bunge la nchi hiyo zitaendelea kusitishwa kwa muda usiojulikana.

Kais Saied alitangaza uamuzi huo wa kurefusha muda wa kusimamishwa shughuli za Bunge la nchi hiyo jana Jumatatu, sanjari na kurefusha pia muda wa kuwaondolea kinga ya kushtakiwa wabunge wa nchi hiyo.

Kadhalika Rais wa Tunisia bila kutoa maelezo ya kina, amesema atalihutubia taifa ndani ya siku chache zijazo. Anatazamiwa kuzungumzia mgogoro wa kisiasa na kiuchumi unaoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Nchi ya Tunisia ilitumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya Rais huyo kumfuta kazi Waziri Mkuu, kusimamisha shughuli za Bunge na kutwaa madaraka yote ya nchi mnamo Julai 25.

Bunge la Tunisia

Kais Saied alisema sababu ya maamuzi hayo ni utendaji mbaya wa serikali katika suala la kupambana na maambukizi ya corona na hali mbaya ya kiuchumi. Hata hivyo kambi ya upinzani inasema maamuzi hayo yanabana uhuru na demokrasia.

Aidha Spika wa Bunge la Tunisia lililosimamishwa, Rached Ghannouchi amesema hatua aliyochukua Rais Kais Saied ni mapinduzi dhidi ya mapinduzi ya wananchi, katiba ya nchi na uhuru wa taifa. Vilevile Rais wa zamani wa Tunisia Moncef Marzouki amekosoa sera na maamuzi ya Rais Kais Saied na kusema hatua hizo ni sawa na mapinduzi na udikteta na kwamba ni ufisadi mbaya zaidi.