Wahajiri 17 wafariki dunia katika ajali ya boti pwani ya Libya
(last modified Tue, 24 Aug 2021 07:47:36 GMT )
Aug 24, 2021 07:47 UTC
  • Wahajiri 17 wafariki dunia katika ajali ya boti pwani ya Libya

Shirika la Wahamiaji Duniani (IOM) limesema wahajiri 17 wamekufa maji baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya Libya.

Safa Msehli, msemaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa amesema boti hiyo iliyokuwa imebeba wahajiri wapatao 70, ilizama usiku wa kuamkia jana katika mji wa Zuwara, magharibi mwa Libya, huo ukiwa ni muendelezo wa matukio ya kufa maji wahajiri wakiwa katika safari hatarishi za kujaribu kuelekea Ulaya.

Amesema Gadi ya Pwani ya Libya imefanikiwa kuwaokoa wajahiri 51 raia wa Misri katika tukio hilo, mbali na kuopoa mwili mmoja katika Bahari ya Mediterania, huku maiti 16 zikikosekana na hivyo wahajiri hao kuhesabiwa kuwa wameaga dunia.

Wiki iliyopita, taarifa ya pamoja ya Shirika la Wahamiaji Duniani (IOM) na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ilithibitisha kuwa watu 47 wamefariki dunia katika ajali nyingine ya boti iliyotokea katika pwani ya bahari ya Atlantiki ya Afrika Kaskazini.

Safari hatarishi za baharini za kujaribu kufika Ulaya kusaka maisha mazuri

Kuanzia Januari mwaka huu, zaidi ya watu 350 wamepoteza maisha, wakati zaidi ya wakimbizi 8,000 na wahamiaji wamefika Uhispania wakitumia njia hii ya baharini.

Aghalabu ya wahajiri hao haramu ambao kutokana na sababu za kiuchumi na usalama huamua kuziacha nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, wanatokea katika nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia.