Kurefusha Rais wa Tunisia muda wa kusimamishwa shughuli za Bunge
Licha ya malalamiko ya kila upande, lakini Rais wa Tunisia Kais Saied ametangaza kuwa, shughuli za Bunge la nchi hiyo zitaendelea kusitishwa kwa muda usiojulikana.
Tunisia ilitumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo kumfuta kazi Waziri Mkuu, kusimamisha shughuli za Bunge, kuondoa kinga ya kisiasa kwa Wabunge na kutwaa madaraka yote ya nchi.
Hatua hizo za Rais wa Tunisia zilikabiliwa na malalamiko ya wananchi wengi wa nchi hiyo, vyama vya siasa na viongozi wa taifa hilo. Wananchi wa Tunisia wanasema kuwa, hatua hizo ni kinyume kabisa na katiba pamoja na mwenendo wa demokrasia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hii ni katika hali ambayo, akiwa na lengo la kutetea hatua zake hizo, Rais Kais alisema kuwa, amechukua uamuzi huo ili kukabiliana na usimamizi mbaya wa kiuchumi na uongozi mbovu katika sekta ya afya hasa baada ya kusambaa virusi vya Corona.
Rais Kais ametangaza kuwa, muda si mrefu ataunda serikali ambayo inaendana na irada na matakwa ya wananchi wa Tunisia, huku akisisitiza kwamba, hatorejea nyuma na kulegeza kamba katika maamuzi aliyoyachukua.

Rais Kais Saied amedai kwamba, hatua alizochukua ni kwa mujibu wa kipengee cha 80 cha Katiba ya Tunisia ambacho kinaeleza wazi kwamba, endapo usalama wa taifa, mamlaka ya nchi na ardhi ya taifa vitakuwa hatarini na ikashindikana kuyatatua hayo katika mazingira ya kawaida basi Rais anaweza kuvunja Bunge. Kipengee hicho kinatumika pia katika mazingira ya hali ya hatari. Hata hivyo wapinzani wanapinga hoja za Rais huyo na wanasisitiza kwamba, hatua alizochukua rais zinakiuka bayana kabisa Katiba ya nchi.
Rais wa Tunisia amechukua hatua hizo na kung'ang'ania maamuzi yake katika hali ambayo, kwa muda nchi hiyo ilikuwa ikishuhudia mvutano wa siri na dhahiri baina yake na Waziri Mkuu pamoja na chama kikuu cha kisiasa nchini humo cha al-Nahdha ambacho kina nafasi kubwa na muhimu katika muundo wa madaraka katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Filihali pia, akthari ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, hatua na maamuzi hayo ya Rais wa Tunisia yanalenga kuishinikiza al-Nahdha na ni mkakati wa kutaka kukiondoa chama hicho katika ulingo wa siasa za nchi.
Anga ya sasa ya kisiasa nchini Tunisia na kupamba moto mizozo na hitilafu, kumepelekea kuongezeka uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Imarati, Misri na Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi ambazo zipo katika medani ya siasa za Tunisia.

Kuhusiana na hilo, Rashid al-Ghanoushi, Spika wa Bunge la Tunisia aliyeuzuliwa, amekosoa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ambapo mbali na kuashiria hatua ya Imarati ya kuunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na Rais Kais Saied ya kuvunja Bunge na kufanya juhudi za kutwaa na kuhodhi madaraka yote ya nchi amesema: Imarati inaona mirengo yenye muelekeo wa Kiislamu kuwa ni tishio kwake na inaona ni jukumu lake kung'oa mizizi ya mapinduzi na vuguvugu la wananchi pale pale lilipoanzia yaani nchini Tunisia.
Katika hali ambayo, kuendelea mgogoro wa sasa huko Tunisia siyo kwa maslahi ya taifa wala vyama vya siasa hasa katika mazingira ya hivi sasa, Rais Kais Saied amejitokeza tena na kuchukua uamuzi wa kurefusha muda wa kusimamishwa shughuli za Bunge. Inaonekana kuwa, mgogoro wa sasa wa Tunisia umezidi kukita mizizi ,na kuendelea mkwamo huu wa kisiasa, kutakuwa ni tatizo kubwa kwa nchi hiyo katika njia ya kufikia malengo yake hususan katika uga wa kuimarisha demokrasia.