Waislamu Kenya walaani MUHURI kuajiri ‘mtetezi wa mashoga’
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i74156-waislamu_kenya_walaani_muhuri_kuajiri_mtetezi_wa_mashoga’
Waislamu nchini Kenya wameliomba Baraza Kuu la Waislamu nchini humo (SUPKEM) liingilie kati kuhusu uamuzi wa shirika la kutetea haki za Waislamu la Muslims for Human Rights (MUHURI) wa kuajiri Mkurugenzi Mkuu anayedaiwa kuwa mtetezi wa wapenzi wa jinsia moja.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 01, 2021 07:32 UTC
  • Waislamu Kenya walaani MUHURI kuajiri ‘mtetezi wa mashoga’

Waislamu nchini Kenya wameliomba Baraza Kuu la Waislamu nchini humo (SUPKEM) liingilie kati kuhusu uamuzi wa shirika la kutetea haki za Waislamu la Muslims for Human Rights (MUHURI) wa kuajiri Mkurugenzi Mkuu anayedaiwa kuwa mtetezi wa wapenzi wa jinsia moja.

Katika barua iliyoandikwa kwa Mwenyekiti wa MUHURI, Khelef Khalifa, waumini wa dini ya Kiislamu wamesema wamekerwa sana na hatua ya MUHURI. Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo linalochapishwa nchini Kenya.

Sehemu ya barua hiyo inasema, “Sisi kama Waislamu wa Kaunti ya Mombasa na Kenya kwa jumla, tumehuzunishwa sana na hatua ya hivi majuzi ya kumwajiri Mkurugenzi Mkuu mpya katika MUHURI. Tunakashifu vikali uamuzi uliochukuliwa na bodi ya shirika hilo kumwajiri mtu anayeenda kinyume na maadili ya dini yetu."

Walalamishi walisema hawatakaa kimya na kukubali shirika linalotumia jina la Uislamu kuendeshwa kwa misingi ya itikadi ambazo zinaenda kinyume na mafundisho ya dini hiyo tukufu. Imefafanua kwa kusema, “Hatua iliyochukuliwa inayonyesha wazi kwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu. Tunataka bodi iitishe kujiuzulu kwa mkurugenzi mkuu mpya mara moja."

Mwenyekiti wa MUHURI, Khelef Khalifa

Waislamu hao wamemtaka Bw Khalifa abadilishe jina la MUHURI ili likome kuhusishwa na Uislamu. Bila hilo, wametishia kuitisha maandamano ili kukemea wazi mienendo ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu.

Mapema mwezi huu, MUHURI ilitangaza kumwajiri Bi Marie Ramtu kuwa mkurugenzi mkuu mpya. Bi Ramtu aliwahi kufanya kazi katika shirika la kutetea haki za binadamu la Network of African National Human Rights Institution (NANHRI). Aliwahi pia kuhudumu katika shirika la Church World Service, ambapo inasemekana alihudumu kulinda masilahi ya watu walio hatarini kudhulumiwa kingono au kijinsia.