Wafanyakazi, viongozi wa kisiasa Tunisia wakataa kukutana na Maseneta wa US
Muungano mkubwa zaidi wa wafanyakazi nchini Tunisia UGTT na vyama viwili vya kisiasa nchini humo vimesusia mwaliko wa ujumbe wa Maseneta wa Marekani ulioitembelea nchi hiyo ya Kiarabu, kujadili mgogoro na mkwamo wa kisiasa unaoshuhudia nchini humo.
Sami Tahri, msemaji wa UGTT amekosoa vikali uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa, "Masuala yetu Watunisia yanapaswa kutatuliwa na sisi Watunisia wenyewe."
Amesisitiza kuwa muungano huo hautashiriki mkutano unaotazamiwa kufanyika leo Jumamosi katika ubalozi wa Marekani mjini Tunis. Tahri ameeleza bayana kuwa, "UGTT haikukubali kuburuzwa na nchi ajinabi wakati wa utawala wa rais wa zamani, Zainul Abiddin Ben Ali, na kamwe haitakubali hilo leo wala kesho."
Wakati huo huo, chama cha 'Katiba Huru' kinachoongozwa na Abir Moussi, muungaji mkono wa zamani wa Ben Ali, kile cha Achaab kilichokaribu na rais wa sasa wa Tunisia vimesema havitashiriki mkutano huo wa ujumbe wa Maseneta wa Marekani vikisisitiza kuwa, haviungi mkono masuala ya ndani ya nchi hiyo kutatuliwa na nchi ajinabi.
Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ilitumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo kumfuta kazi Waziri Mkuu, kusimamisha shughuli za Bunge, kuondoa kinga ya kisiasa kwa Wabunge na kutwaa madaraka yote ya nchi.
Licha ya malalamiko ya kila upande, lakini rais huyo wa Tunisia mwezi uliopita alitangaza kuwa, shughuli za Bunge la nchi hiyo zitaendelea kusitishwa kwa muda usiojulikana.