Tunisia yasikitishwa na uamuzi wa Ufaransa wa kupunguza viza kwa raia wake
Rais Kais Saied wa Tunisia amefanya mazungumzo na simu na Rais mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kueleza kusikitishwa na umauzi uliochukuliwa na Paris wa kupunguza idadi ya viza zilizokuwa zikitolewa kwa raia wa Tunisia wanaotaka kuelekea Ufaransa.
Ofisi ya Rais wa Tunisia imeeleza kuwa, hatua hiyo ya Paris inaweza kubadilishwa.
Rais Kais Saeid wa Tunisia amesema kuwa suala la uhajiri usio wa kawaida linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa msingi wa mtazamo mpya na kwamba hilo litakuwa moja ya vipaumbele vya serikali mpya ya Tunisia.
Katika mazungumzo hayo ya simu marais wawili wa Ufaransa na Tunisia wamejadili masuala ya uhamiaji na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika uwanja huo.
Jumanne iliyopita Paris ilitangaza kupunguza idadi ya viza ambazo imekuwa ikitoa kwa raia wa Morocco, Algeria na Tunisia ikisema kuwa imefanya hivyo kutokana na nchi hizo za kaskazini mwa Afrika kukataa kutoa vibali vinavyohitajika kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani wahajiri waliokatiliwa nchini Ufaransa.
Mbali na suala hilo la viza, marais wa Ufaransa na Tunisia wamejadili pia kuhusu Mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa (OIF) uliopangwa kufanyika katika mji wa Djerba huko Tunisia tarehe 20 hadi 21 mwezi Novemba mwaka huu. Wamejadiliana kuhusu maandalizi ya mkutano huo na kadhia zitakazojadiliwa katika mkutano huo ujao kati ya Rais Saeid na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Bi Louise Mushikiwabo kutoka Rwanda.