Nov 23, 2021 07:35 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia kuingia katika medani ya vita kukabiliana na TPLF

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza kuwa leo atajitosa kwenye medani ya vita kati ya vikosi vya serikali ya nchi hiyo na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Abiy alisema hayo jana katika taarifa aliyoituma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa: Kuanzia kesho (leo Jumanne) nitaongoza vikosi vyetu vya ulinzi nikiwa mstari wa mbele. 

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019 ameongeza kuwa: Wanaotaka kuwa miongoni mwa watoto wa Ethiopia ambao watanyanyuliwa na historia, inukeni kwa ajili ya nchi yenu leo. Tukutane katika mstari wa mapambano.

Hata hivyo viongozi wa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamepuuzilia mbali matamshi hayo ya Abiy Ahmed, wakisisitiza kuwa ni dhihaka na poroji isiyo na umuhimu wowote.

Mapigano eneo la Tigray

Haya yanajiri huku mapigano makali yakiendelea kuripotiwa baina ya jeshi la Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) katika maeneo ya magharibi katika mpaka na jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.

Mapigano katika jimbo la Tigray yanashadidi katika hali ambayo, indhari mbalimbali zimeendelea kutolewa kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika jimbo hilo.

Vita hivyo vya kaskazini mwa Ethiopia vya karibu mwaka mmoja sasa vimepelekea watu maelfu ya watu kuuawa, zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi na kuwafanya wengine zaidi ya laki nne kukabiliwa na baa la njaa.

Tags