Zaidi ya Walibya elfu tano wajitokeza kugombea viti vya Bunge nchini Libya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya imetangaza kuwa, faili la kuandikisha majina ya wagombea wa viti vya Bunge limefungwa na kwamba zaidi ya Walibya elfu tano wamejiandikisha kwa ajili ya kugombea viti hivyo.
Taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya imesema watu elfu tano na 385 wamejiandikisha kwa ajili ya kuwania viti vya Bunge na kwamba nyaraka zilizowasilishwa na wagombea hao zitaanza kuchunguzwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Wakati huo huo mjumbe aliyejiuzulu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Jan Kubis, amewatumia ujumbe wananchi wa Libya akieleza sababu za uamuzi wake wa kuacha nafasi hiyo na kumtakia mafanikio Stephanie Williams, mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Libya.
Katika ujumbe huo, Kubis amesisitiza kuwa, kufanyika kwa uchaguzi huru na wa uwazi wa wabunge na rais kwa wakati ufaao ni muhimu sana ili kukamilisha kipindi cha mpito, kurejea katika demokrasia na kujenga nchi iliyoungana na yenye mamlaka na uhuru.
Itakumbukwa kwamba, Baraza Kuu la Serikali ya Libya jana Alkhamisi lilipendekeza kuwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ufanyike mwezi Februari mwakani sawa na ule wa Bunge badala ya tarehe 24 Disemba mwaka huu.
Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi Libya, Omar Abdel Aziz Bushah ameashiria mivutano iliyopo, hali ya kutoaminiana iliyopo baina ya vyama vya kisiasa na uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kutahadharisha kuwa, hali ya mambo nchini Libya itavuruga mchakato mzima wa kisiasa wa nchi hiyo.