Afisa mwandamizi wa Annahdha 'atekwa nyara' na maafisa usalama Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78700-afisa_mwandamizi_wa_annahdha_'atekwa_nyara'_na_maafisa_usalama_tunisia
Harakati ya Annahdha nchini Tunisia imesema kuwa, afisa mwandamizi wa chama hicho cha kisiasa ametiwa mbaroni na maafisa usalama wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 01, 2022 09:04 UTC
  • Afisa mwandamizi wa Annahdha 'atekwa nyara' na maafisa usalama Tunisia

Harakati ya Annahdha nchini Tunisia imesema kuwa, afisa mwandamizi wa chama hicho cha kisiasa ametiwa mbaroni na maafisa usalama wa nchi hiyo.

Taarifa ya chama hicho kikubwa zaidi cha siasa nchini Tunisia imelaani vikali kitendo cha kukamatwa Noureddine Bhiri, aliyekuwa Waziri wa Sheria, na pia naibu rais wa chama hicho maarufu cha kisiasa.

Samir Dilou, mwanasheria na mbunge wa zamani wa Tunisia amesema afisa huyo wa ngazi ya juu wa Annahdha alikamatwa jana jijini Tunis, na maafisa usalama waliokuwa wamevaa mavazi ya kiraia, wakati akitoka nyumbani kwake akiwa ameandamana na mkewe.

Rais Kais Saeid wa Tunisia

Dilou amesema, maafisa hao walimkamata kwa mabavu na kumpelekea kusikojulikana kiongozi huyo wa chama hicho cha Kiislamu nchini Tunisia, mbali na kutwaa kwa nguvu simu ya rununu ya mkewe, Saida Akremi. Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na serikali ya Tunis kuhusu kukamatwa kwa Bhiri kufikia sasa.

Tunisia ilitumbukia katika mivutano na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu tarehe 25 Julai mwaka uliomalizika, wakati Rais wa nchi hiyo, Kais Saied alipoanza kuchukua maamuzi yanayotajwa kuwa yanapingana na Katiba ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli za Bunge, kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria, kumuuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo na kuhodhi madaraka yote ya nchi.

Makundi na vyama vya siasa nchini Tunisia vimeendelea kupinga maamuzi hayo vikiyataja kuwa ni mapinduzi dhidi ya Katiba.