Miito yatolewa Tunisia kwa ajili ya kuachiwa huru Naibu Mkuu wa Annahdha
Miito imeendelea kutolewa nchini Tunisia ili kuachiwa huru mwanasiasa aliyeko kizuini, Noureddine Bhiri, ambaye pia ni Naibu Mkuu wa chama kikubwa zaidi cha kisiasa huko Tunisia cha Annahdha.
Maafisa usalama wa Tunisia waliokuwa katika mavazi ya kiraia Ijumaa iliyopita walimtia nguvuni katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis, Noureddine Bhiri aliyewahi kuwa waziri wa Sheria wa Tunisia. Bhiri alikamatwa na askari kanzu hao akitoka nyumbani.
Tume Huru ya Taifa ya Kukabiliana na Mateso Tunisia (INPT) imeeleza kuwa, maafisa usalama hawajatoa taarifa yoyote kuhusu hali ya Bhiri au Fathi Baldi, afisa wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo ambaye pia alichukuliwa kwa ajili ya mahojiano juzi Ijumaa.
Mkuu wa Tume Huru ya Taifa ya Kukabiliana na Mateso Tunisia (INPT) Fathi al Jarray amesema kuwa, hadi sasa Wizara ya Mambo ya Ndani haijatoa jibu kwa ombi lao la kutaka kujua mahali walipo wanasiasa hao wawili.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, chama cha Annahdha kimekuwa na nafasi kuu katika siasa za Tunisia hadi Rais wa sasa wa nchi hiyo Kais Saied alipohodhi madaraka ya nchi hiyo mwezi Julai mwaka huu.
Tunisia inatajwa kuwa ndio nchi pekee iliyoweza kurejesha utawala wa kidemokrasia baada ya mapinduzi ya wananchi yaliyoshuhudiwa katika nchi kadhaa za Kiarabu za kaskazini mwa Afrika miaka kumi iliyopita. Hata hivyo makundi ya kiraia na wapinzani wa Rais wa sasa wa Tunisia wameeleza hofu na wasiwasi wao juu ya uwezekano wa nchi hiyo kurejea katika utawala wa kibabe na kidikteta, muongo mmoja baada ya mapinduzi ya wananchi yaliyomuondoa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali.
Tunisia ilitumbukia katika mivutano na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu tarehe 25 Julai mwaka uliomalizika, wakati Rais wa nchi hiyo, Kais Saied alipoanza kuchukua maamuzi yanayotajwa kuwa yanapingana na Katiba ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli za Bunge, kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria, kumuuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo na kuhodhi madaraka yote ya nchi.
Makundi na vyama vya siasa nchini Tunisia vimeendelea kupinga maamuzi hayo vikiyataja kuwa ni mapinduzi dhidi ya Katiba.