Chama cha Ennahda Tunisia chatoa wito wa maandamano makubwa Ijumaa ijayo
Chama cha Ennahda chenye mfungamano na Harakati ya Ikhwanul Muslimini cha Tunisia kimetoa taarifa kikiwatolea wito wananchi kushiriki kwa wingi katika maandamano yatakayofanyika nchini humo Ijumaa tarehe 14 mwezi huu wa Januari.
Chama hicho kimetangaza kuwa, kinawatolea wito wanamapambano na makundi yote ya kijamii nchini Tunisia kushiriki kwa wingi katika maandamano hayo ya Ijumaa wiki hii ambayo inasadifiana na siku ya kumbukumbu ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011.
Rais Kais Saeid wa Tunisia amebadili tarehe ya kumbukumbu ya mapinduzi ya wananchi ya Tunisia na kuifanya Disemba 17 badala ya Januari 14 na kutangaza kuwa tarehe hiyo ya awali haifai.
Tunisia imekuwa na mfumo mseto unaogawa madaraka baina ya Rais na Bunge tangu baada ya mapinduzi ya 2011 na suala hilo limepelekea kuongezeka hali ya mivutano kati ya mihimili miwili ya dola kuhusu mamlaka ya kisheria.