Chama cha Nahdha Tunisia chataka kuhitimishwa ukandamizaji dhidi ya waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79244-chama_cha_nahdha_tunisia_chataka_kuhitimishwa_ukandamizaji_dhidi_ya_waandamanaji
Chama cha Nahdha cha Tunisia kimetoa taarifa kikitaka kuhitimishwa vitendo vya utumiaji mabavu na ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 15, 2022 23:15 UTC
  • Chama cha Nahdha Tunisia chataka kuhitimishwa ukandamizaji dhidi ya waandamanaji

Chama cha Nahdha cha Tunisia kimetoa taarifa kikitaka kuhitimishwa vitendo vya utumiaji mabavu na ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo.

Sambamba na kulaani ukandamizaji huo, Harakati ya Nahdha imetoa wito wa kuachiliwa huru wananchi waliotiwa mbaroni katika maandamano ya kulalamikia serikali ya sasa ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Kais Saied.

Sehemu nyingine ya taarifa ya chama hicho imelaani vikali sheria kali na marufuku iliyowekwa na vyombo vya usalama dhidi ya maandamano ya amani ya wananchi ambayo lengo lake ni kutetea uhuru wa kutoa maoni.

Tunisia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Januari 25 mwaka uliopita 2021. Rais Kais Saied wa nchi hiyo alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika wa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha kuchukua udhibiti wa masuala yote ya nchi.

Maandamano ya wananchi wa Tunisia

 

Tangu wakati huo,  wananchi wa Tunisia wamekuwa wakimiminika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Tunisia, Tunis katika maandamano ya kumtaka rais huyo ajiuzulu. Juzi  Ijumaa pia, polisi ya Tunisia ilitumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuvunja maandamano ya wananchi dhidi ya Rais Saeid.

Wananchi wengi wa Tunisia wanaamini kwamba hatua za Saied zinapingana na malengo ya vuguvugu la wananchi na kwamba zitarejesha tena udikteta nchini Tunisia. Wengi wao wana wasiwasi kwamba, mustakabali wa nchi hiyo utaangukia tena mikononi mwa wale wanaoendeleza njia ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali.