Umoja wa Mataifa waelezea kusikitishwa na hali mbaya ya kisiasa nchini Tunisia
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kufuatia kuongezeka ukandamizaji wa wapinzani nchini Tunisia sambamba na wakati huu wa kuadhimisha mapinduzi ya wananchi yaliyomng'oa madarakani dikteta Zainul Abidin Ben Ali.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ameelezea wasiwasi wake huo na kusema kuhusu hatua ya Rais Kais Saied wa Tunisia ya kumfuta kazi Waziri Mkuu na kulivunja Bunge kwamba mapinduzi ya nchini Tunisia yalitia matumaini ya kuheshimiwa demokrasia katika nyoyo za walimwengu na hivi sasa tunasisitiza kwamba, misingi ya demokrasia lazima iheshimiwe.
Itakumbukwa kuwa jana Ijumaa, jeshi la polisi nchini Tunisia kwa mara ya kwanza kabisa lilitumia maji yenye sumu na gesi ya kutoa machozi pamoja na marungu kutawanya waandamanaji wakati walipokuwa wanaadhimishwa mapinduzi yao ya mwaka 2011.
Wiki iliyopita pia, chama cha al Nahdha cha Tunisia kilitoa taarifa kikitaka kuhitimishwa vitendo vya utumiaji mabavu na ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo.
Sambamba na kulaani ukandamizaji huo, Harakati ya al Nahdha ilitoa wito wa kuachiliwa huru wananchi waliotiwa mbaroni katika maandamano ya kulalamikia serikali ya sasa ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Kais Saied.
Sehemu nyingine ya taarifa ya chama hicho ililaani vikali sheria kali na marufuku iliyowekwa na vyombo vya usalama dhidi ya maandamano ya amani ya wananchi ambayo lengo lake ni kutetea uhuru wa kutoa maoni.
Tunisia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Januari 25 mwaka uliopita 2021. Rais Kais Saied wa nchi hiyo alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha kuchukua udhibiti wa masuala yote ya nchi.