May 28, 2016 07:51 UTC
  • 5 wahukumiwa maisha jela Uganda kwa mashambulizi ya kigaidi Kampala

Mahakama Kuu ya Uganda imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela, watu watano miongoni mwa wanane waliopatikana na hatia ya kuhusika katika mashambulizi pacha mjini Kampala, wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.

Watano hao ni Issa Ahmed Luyima (Uganda), Hussein Hassan Agad maarufu Hussein Agade (Tanzania), Idris Magondu kwa jina jingine Christopher Magondu (Kenya), Habib Suleiman Njoroge (Kenya) na Mohamed Ali Mohamed (Tanzania). Jaji wa Mahakama Kuu Alphonse Owiny Dollo, amesema mashambulizi hayo ya kigaidi yalilenga raia wasio na hatia na mbali na kusababisha vifo vya makumi ya watu, wengine wengi walikuwa vilema na baadhi wanaendelea kuuguza majeraha zaidi ya miaka mitano baada ya hujuma hiyo. Akisoma hukumu hiyo ya dakika 13 jana Ijumaa, Jaji Dollo amesema waliohusika katika hujuma hizo walisukumwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia, kulipiza kisasi hatua ya Uganda kutuma askari wake wa UPDF katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwaka 2007, kufanya kazi chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM. Washukiwa wengine wawili wamehukumiwa kifungo cha miaka 50 jela huku mmoja kwa jina Muzafar Luyima, akitolewa hukumu ya kutumikia jamii kwa muda wa mwaka mmoja, baada ya kuwekwa rumande kwa miaka 6 katika gereza la Luzira, kinyume na miaka mitatu kama inavyotakiwa na sheria za nchi hiyo.

Watu 76 walipoteza maisha katika mashambulizi ya kigaidi dhidi ya ukumbi wa mchezo wa Raga katika mtaa wa Lugogo na mgahawa wa Kiethiopia eneo la Kabalagala, viungani mwa mji mkuu Kampala, wakizatazama fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, kati ya Uhispania na Uholanzi.

Tags