Wakenya wengine watatu wauliwa na ash Shabab
Mkuu wa Jeshi la Polisi la eneo la Pwani nchini Kenya ametangaza habari ya kuuawa raia kadhaa wa nchi hiyo, jana asubuhi.
Shirika la habari la Xihnua limemnukuu Francis Wanjohi akisema kuwa, wanamgambo waliojitoa kwenye kundi la ash Shabab waliua Wakenya watatu jana asubuhi katika mji wa Kwale wa kusini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Wanjohi, Wakenya hao watatu walikuwa wakilinda usalama wa wakazi wa mji wa Kwale na wameuliwa katika maeneo matatu tofauti ya mji huo.
Mkuu huyo wa jeshi la polisi la eneo la Pwani huko Kenya amesisitiza kuwa, wanamgambo waliofanya mauaji hayo bado wanasakwa pamoja na wanamgambo wengine wa ash Shabab waliorejea nchini Kenya kutokea Somalia.
Wanjohi ameongeza kuwa, karibu vijana 300 wa Kenya ambao walijiunga na kundi la ash Shabab nchini Somalia, wamerejea nchini Kenya hivi sasa na jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka.