Wanachama wa genge moja la kigaidi watiwa mbaroni nchini Tunisia
Askari usalama nchini Tunisia wametangaza kuwa, wamefanikiwa kusambaratisha mtandao mmoja wa kigaidi ujulikanao kwa jila la "al Muwahhidun" katika miji wa Tataouine na Soussa ya kusini mwa mji mkuu Tunis.
Tunisia imeamua kuchukua hatua zaidi za tahadhari baada ya kuongezeka wasiwasi wa kurejea tena magenge ya kigaidi na ukufurishaji huko kaskazini mwa Afrika.
Duru za kieneo zimetangaza leo Jumatano kwamba askari wa kupambana na vitendo vya kigaidi kutoka gadi ya taifa kwa kushirikiana na idara ya mahakama wamefanikiwa kugundua genge hilo la ukufurishaji la kulisambaratisha katika miji hiyo miwili ya Tunisia.
Maficho makuu ya genge hilo yalikuwa katika mji wa Tataoune na kiongozi wake ni gaidi mkufurishaji ambaye alikuwa akisakwa. Taarifa hizo zimeongeza kuwa, genge hilo lilikuwa na mfungamano wa moja kwa moja na kundi la kigaidi la Daesh yaani ISIS.
Mwanzoni mwa mwei huu wa Machi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia ilitangaza kuwa, idara ya kupambana na ugaidi katika gadi ya taifa ya nchi hiyo imefanikiwa kutia mbaroni magaidi 55 wakufurishaji pamoja na viongozi wao.
Tangu baada ya wananchi wa Tunisia kufanikisha mapinduzi yao yaliyomng'oa madarakani dikteta Zine El Abidine Ben Ali mwaka 2010 hadi hivi sasa, magenge ya ukufurishaji yamekuwa yakifanya vitendo mbalimbali vya kigaidi nchini humo. Moja ya sababu kuu za kuendelea ugaidi wa magenge hayo ni njama za kutaka nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika isiwe na utulivu hata kidogo na wala mapinduzi ya wananchi yasiwe kigezo kwa nchi nyingine za Kiarabu.
Tunisia inapakana na nchi kama Libya ambayo haina utulivu wa kisiasa na hilo linahesabiwa kuwa moja ya sababu za kuendelea vitendo vya kigaidi nchini Tunisia.