Miili 20 ya wahajiri yaopolewa baharini pwani ya Tunisia
Wapiga mbizi na maafisa usalama wa Tunisia jana Jumamosi waliopoa miili ya watu wengine wanane baada ya boti yao kuzama katika pwani ya nchi hiyo, na kufikisha idadi ya maiti zilizoopolewa hadi sasa kufikia 20.
Shirika la habari la Xinhua limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, shughuli ya kutafuta miili ya wahajiri wengine wanaoaminika kuzama katika pwani ya Nabeul kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ingali inaendelea.
Kwa mujibu wa Radio ya Shems FM ya Tunisia, aghalabu ya wahajiri haramu walioaga dunia baada ya chombo chao cha kusafiria kuzama katika Bahari ya Mediterania huenda walikuwa raia wa Syria.
Hata hivyo maafisa wa serikali ya Tunisia wamesema wameanzisha uchunguzi kubaini utambulisho na uraia wa wahajiri hao waliokufa maji katika pwani ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Wakuu wa Tunisia hutekeleza oparesheni karibu kila siku kuwazuia wahajiri wanaotumia nchi hiyo kuvuka Bahari ya Mediterrania kuelekea barani Ulaya kinyume cha sheria.
Takwimu za Shirila la Kimataifa la Wahajiri (IOM) zinaonesha kuwa, wahajiri karibu 3,000 walikufa maji baharini wakati wakijaribu kuelekea barani Ulaya kwa kutumia maeneo ya kaskazini mwa Afrika mwaka jana 2021, na hiyo ilikuwa ni ongezeko la asilimia 155 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.
Idadi kubwa ya wahajiri hao walipoteza maisha katikati ya Bahari ya Mediterania wakiwa wametokea Tunisia, Algeria, Libya na Morocco.